Makala

SAUTI YA MKEREKETWA: Tunawaenzi mabalozi hawa wa Kiswahili katika mabunge ya kitaifa, Seneti

September 23rd, 2020 2 min read

Na HENRY INDINDI

ANAVYONUKULIWA na Ustadh Wallah bin Wallah katika Malenga wa Ziwa Kuu, Rais wa awamu ya tatu, Mhe Mwai Kibaki aliyasema haya mwaka 1984: “Maadamu serikali ambayo ndiyo rubani wa taifa imekwisha tangaza rasmi kwamba Kiswahili ni lugha ya taifa, basi pasiwepo woga wowote katika kuitumia. Kilichobaki sasa ni juu ya kila mwananchi kushiriki kwa kila hali na kukuza lugha yenyewe. Hasa walimu wawe mstari wa mbele kuwafunza vijana wetu lugha sanifu. Na endapo patakuwa na shida yoyote au kikwazo chochote katika harakati za kukuza lugha hii, basi serikali iarifiwe itoe msaada unaohitajika.”

Aliyasema katika ufunguzi rasmi wa kongamano la ukuzaji wa Kiswahili. Enzi hizo viongozi wakuu serikalini wangehudhuria makongamano ya Kiswahili, siku hizi ni kama viwango vya uzalendo vilishuka.

Na leo tunateua kuwasherehekea baadhi ya wanasiasa wanaotusaidia kudhihirisha kwamba Kiswahili kinaweza kutekeleza majukumu ya kitaifa.

Wabunge na maseneta hawa hukizungumza Kiswahili kwa fahari kubwa licha ya wenzao wengi kuonea fahari matumizi ya Kiingereza bungeni. Hili kwa hakika linatushawishi kuwapongeza, kuwashajiisha, kuwahimiza, kuwaonea fahari na kuwashukuru.

Katika bahari pana ya samaki wala watu, ukipata samaki muokoa watu usikose kumtambua na kumwonea fahari. Ndivyo ilivyo kwa hawa tunaotabarukia Sauti ya Mkereketwa leo.

Hawa ndio wanaodhihirisha hasa thamani ya matakwa wanayohitajika kutimiza ya kuwa na uwezo wa kujieleza katika Kiswahili kabla ya kuidhinishwa kuwania nyadhifa hizo.

Ndio wanaoelewa thamani ya uzalendo kwa taifa na thamani ya lugha ya taifa hasa. Wamekataa kufungiwa katika pingu za wakoloni kwamba lugha za Kiafrika haziwezi kutekeleza majukumu muhimu ya kitaifa hata zikipewa nguvu na mamlaka ya kitaifa. Hawa tu ndio wanaojitahidi kutuondolea aibu ya kuwa na mabunge ya taifa yanayojadili masuala ya kitaifa katika lugha za kikoloni /kigeni huku kukiwa na lugha ya taifa. Hatuwezi kupata zawadi nyingine kubwa ila kuwashukuru hapa na kuwahimiza wazidishe kani katika hilo. Waendelee kutuondolea aibu hiyo.

Ingawa wapo wanaotoka Pwani kama Stewart Madzayo (Kilifi), Issa Boy (Kwale), Mwinyi Mohammed (Mombasa), Mohammed Ali (Nyali), Mishi Mboko (Likoni) na Abdulswamad Nassir (Mvita), kuna wenzao wa kutoka bara ambao kwa hakika wameonesha mfano wa kuigwa.

Maseneta Isaac Mwaura (maalum) na John Kinyua (Laikipia) huzungumza Kiswahili kwa kukionea fahari kubwa sana.

Ufasaha wao na mtiririko wa mawazo hunipa matumaini kwamba wapo wanaoweza kutetea Kiswahili na nafasi yake fursa hiyo ikipatikana. Tunawashukuru sana.

Sasa tutatumia fursa hii kuwaomba mabalozi hawa wa Kiswahili, kuanzisha mchakato wa kutunga sheria ya kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya pekee bungeni.

Ndiyo lugha ya taifa na ndiyo inayopaswa kuwa ikitumiwa kujadili masuala ya taifa.

Niliwahi kumdokezea hili Seneta Mwaura katika kongamano la mwisho la Tuzo ya Ubunifu na sasa ni wakati wa kulifufua kwa manufaa ya Kiswahili leo, kesho na keshokutwa. Tunawashukuru sana.