SAUTI YA MKEREKETWA: Usalama wetu na wa watoto shuleni ni jukumu la ubia

SAUTI YA MKEREKETWA: Usalama wetu na wa watoto shuleni ni jukumu la ubia

Na HENRY INDINDI

AKITANGAZA taratibu za kufunguliwa kwa shule hivi majuzi, Waziri wa Elimu, Prof George Magoha alitoa kauli ambayo baadhi ya wahakiki waliibeba kwa moto wa juu kwelikweli.

Yamkini, waziri alisema kwamba katika hali inakuwa vigumu kuepuka kutokaribiana madarasani, walimu wanaweza kutumia njia bunifu na kuwafundishia baadhi ya wanafunzi kwenye vivuli vya miti.

Sijui sababu ya kuvamiwa kwa waziri Magoha kutokana na kauli hii lakini ninaweza kukisia tu kwamba waliomkashifu walimwona kama anayeturejesha katika siku za nyuma sana na ambaye alitangaza kutojipanga kwa serikali zetu kushughulikia mambo muhimu.

Si neno! Waliomkashifu waziri wa elimu wana sababu tena nzuri maanake walitaka kuiminya serikali mashavu na kuikumbusha kuhusu haja ya kujipanga kama taifa kadiri idadi ya watu inavyoendelea kuongezeka.

Hata hivyo, mgonjwa hachapwi. Tunaugua maradhi ya kutojipanga mapema, msituchape fimbo mtatuua. Hali tuliyo nayo sasa ni kwamba hatuna madarasa ya kutosha na hatukuweza kuyajenga madarasa haya ya kutosha licha ya kutanabahishwa na korona. Lakini sasa je, watoto wetu waendelee kukaa nyumbani hadi tutakapojenga madarasa ya kutosha? Sidhani kwamba kuna yeyote anayetaka kuendelea kuwaona watoto hawa nyumbani kutokana na hali tunayoishuhudia.

Waziri Magoha anapopendekeza ubunifu wa kutuwezesha kushona kiraka cha dharura ili watoto wetu wasitaabike shuleni au kujiweka katika hatari ya kuambukizana korona, tusimrajimi kwa mawe.

Ni dharura na tatizo ambalo sharti litafutiwe suluhu. Tunaweza kusaidiana shuleni kufikiria njia mbadala za kulifanikisha hilo la kuwaepushia watoto wetu balaa ya kukaribiana.

Muhimu kwa sasa ni kufikiri kuhusu tunavyoweza kuchanga na kuchangizana kupata kushona kiraka hiki cha dharura na kuwahakikishia watoto wetu usalama shuleni. Kulia na kulalama tu hakutasulushisha tatizo ambalo tayari limetukodolea macho.

Kwa mfano, watahiniwa katika madarasa ya nane na kidato cha nne, wamekuwa shuleni muhula uliopita na nina uhakika asilimia kubwa ya wanafunzi hawa sasa wamekamilisha mahitaji ya silabasi.

Makundi kama haya yanaweza kusomeshewa katika mabwalo kwa masomo ya pamoja na vivulini au katika mahema kwa masomo ya kuteua yasiyo na idadi kubwa ya wanafunzi. Kazi kubwa wanayoifanya sasa ni ya kudurusu na hii bila shaka ikifanyiwa hata kivuni au uwanjani, haitakuwa na tatizo kubwa.

Wengine wanaweza hata kusomeshewa au kufanyia udurusu wao katika maabara na maktaba za shule kwa shule zilizo na majengo kama haya.

Wapo watakaotaja wakati wa maakuli kama utakaokuwa na tatizo. Sidhani kwamba hili pia linapaswa kuwa tatizo kubwa.

Tuwapange wanafunzi wa madarasa mbalimbali kula kwa awamu ili tupunguze kadhia ya watoto kusongamana mahali pamoja kwa kipindi fulani cha wakati. Hakuna tatizo lisilo na suluhu ilmuradi wanaoliona tatizo hilo wahiari kupata suluhu la karibu sana mahali palipo na tatizo hilo kwa gharama ya chini.

Wanafunzi na watoto wetu nao tuwakumbushe haja ya kutilia maanani matumizi ya barakoa na kunawa mara kwa mara shuleni. Tuwakumbushe mara kwa mara kwamba gharama ya kutibu mgonjwa wa korona ni ghali, wasichume majanga watakula na wa kwao.

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Jifunge masombo utafute mali yako ufurahie...

Kaunti ya Mombasa yafuta kazi madaktari 86 akiwemo Chibanzi...