SAUTI YA MKEREKETWA: Viongozi Afrika hawana punje ya ujasiri kwenye kuutumikisha uhuru

SAUTI YA MKEREKETWA: Viongozi Afrika hawana punje ya ujasiri kwenye kuutumikisha uhuru

Na HENRY INDINDI

KATIKA hotuba za kumwomboleza hayati Rais John Pombe Magufuli jijini Dodoma tarehe 22/03/2021 ilikuwa dhahiri kwamba muungwana huyu alipendwa na kuheshimiwa na viongozi wenzake wa Afrika.

Sisi umma wa Kiswahili tulipoteza balozi na shujaa mkubwa aliyejitolea kwelikweli kuhimiza matumizi ya Kiswahili siyo tu katika taifa lake la Tanzania na asasi zake bali pia Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla. Hii ndiyo sababu marais wote waliotoa hotuba hapo ni ama walitoa hotuba katika Kiswahili au kutaja walivyohimizwa na Rais Magufuli kukita matumizi ya Kiswahili katika mataifa yao.

Kwa hivyo huku waombolezaji wakililia uchapakazi wake na jinsi alivyokuwa mzalendo kindakindaki wa Uafrika na thamani yake, sisi tulikuwa wazalendo wapenzi na wakereketwa wa Kiswahili tulikuwa tunakumbushwa tena juhudi za Rais Magufuli katika kueneza Kiswahili duniani. Ilifurahisha kuwaona na kuwasikia marais wa kutoka katika muungano wa mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC), wakisifia juhudi za Rais Magufuli na nia yake ya kuhakikisha kwamba Kiswahili kinafundishwa huko. Wote waliahidi kuendeleza hatua hiyo kama njia ya kumkumbukia na kusema la haki, kutahitajika ‘Magufuli’ mwingine kusukumiza jitihada hiyo.

Nitumie fursa hii kuwapongeza marais Uhuru Kenyatta (Kenya) na mwenzake Felipe Nyusi (Msumbiji) kwa kutoa hotuba zao katika Kiswahili. Ilipunga sana kumsikia Rais wa Msumbiji akitiririsha Kiswahili faridi licha ya kwamba si Mkenya wala si Mtanzania ambao ndio mama na walezi wa Kiswahili. Hili lilitangaza ujumbe wa aina yake kwa yeyote aliyekuwa tayari kusanisi. Wapo watakaosema kwamba Msumbiji ni jirani wa Tanzania kwa hivyo haliwi jambo zito kwa jirani kuijua lugha ya mwenzake, lakini nasi tunawajua majirani wengi hapa na wengine hata wazawa wa mumu humu nchini ambao hata harufu ya Kiswahili hawana.

Rais Nyusi alitudhihirishia kwamba tukiamua kukiuza, kukitangaza na kukieneza Kiswahili kokote hadi nje ya mipaka ya Afrika Mashariki, wenzetu watakipokea na kukifanyia haki.

Sisi tuliozoea kuzisikia hotuba za Kiingereza kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta, tuliufurahia ujasiri wake wa kutoa hotuba yake yote katika Kiswahili hapa. Alijitokeza kuwa mfano bora kwanza kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na pili kama mzawa wa jamii zazi ya Kiswahili. Ingekuwa aibu kubwa kwa mgeni kutoka Msumbiji kutiririsha Kiswahili alivyotiririsha Rais Nyusi na mwenyeji wake wa Afrika Mashariki atorokee katika ukoloni. Nitatumia fursa hii kumwomba Rais Uhuru Kenyatta aendelee na ujasiri huo, na azitoe hotuba zake katika Kiswahili ndani na nje ya nchi.

Huku tukimwombea ufanisi Mama Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni balozi mkubwa sana wa Kiswahili, tunawahimiza wenziwe kutoka Afrika Mashariki waungane naye katika juhudi za kueneza Kiswahili ulimwenguni. Sina shaka kumhusu Mama Samia Suluhu maanake amekuwa akihudhuria makongamano ya Kiswahili bila kukosa. Tunapomwomboleza Rais Magufuli, sisi walezi wa Kiswahili tuwe na matumaini na furaha kwamba alituacha katika mikono salama inayopenda na kuthamini Kiswahili. Tuombee ushirikiano wa kukieneza Kiswahili ulimwenguni.

You can share this post!

Mwanamume anayehusishwa na genge la ‘Jeshi ya...

KAULI YA MATUNDURA: Wataalamu wa Kiswahili wamuenzi...