SAUTI YA MKEREKETWA: Wanetu wafanye kozi za teknolojia ili wasiachwe nyuma kimaisha-leo

SAUTI YA MKEREKETWA: Wanetu wafanye kozi za teknolojia ili wasiachwe nyuma kimaisha-leo

Na HENRY INDINDI

TUNATANGULIZA makala ya leo kwa kuwashukuru na kuwapongeza wanafunzi wote waliovuka vikwazo na ndaro za korona hata wakafanya mitihani ya KCPE na KCSE mwaka huu.

Maadamu matokeo ya mitihani ya kitaifa yashatangazwa na wahitimu wa kiwango hicho wamefahamu sasa uwezo wa kozi za kitaaluma wanazoweza kusomea, tunatabaruku makala ya leo katika kushauriana nao kuhusu mkondo wa ulimwengu wa sasa.

Waliopita na kufanikiwa kujihakikishia kozi za kitaaluma walizotazamia kusomea tunawahongera kwa kufanikiwa kutimiza ndoto na wenzao ambao hawakupata matokeo waliyotumainia kupata pia tunawahimiza kuanzia wanakoweza. Kundi la kwanza lisijione kama linaloweza kuubeba ulimwengu peke yao bali lijue kwamba ulimwengu wetu una matumaini makubwa sana katika uvumbuzi wa vito mbalimbali vitakavyoifaa jamii. Kuanza si kumaliza ingawa ni hatua muhimu ya kumaliza na ndilo wanalopaswa kujikumbusha kila mara.

Waliokosa kupata matokeo waliyotarajia wasikate tamaa na kujihukumu kwa mwisho wa maisha. Wanaoweza kuanzia hata kwenye kozi za vyeti katika vyuo vya kiufundi na vyuo vya anuwai wafanye hivyo bila kusita.

Kila mmoja ana nafasi na mchango wake katika jamii yetu na sote tunategemeana katika taaluma za maishani ili kuafikia ufanisi wa maisha. Kitachokuwa muhimu sana kwao ni nia ya kujiendeleza, nia ya kubadili mustakabali wao maishani, na nia ya kuchangia jambo litakalobadili mkondo wa maisha katika jamii.

Ni muhimu kuwakumbusha kwamba ulimwengu wa sasa unasukumwa na kani za kiteknolojia na kila jambo linahitaji nguvu za kiteknolojia katika kulifanikisha.

Maadamu huku ndiko unakoelekea ulimwengu, watoto wetu na ndugu zetu wasigande kwenye taaluma zilizozoeleka awali bali wawazie mikondo mingine ya kitaaluma itakayotumikisha nguvu hizi za kiteknolojia.

Sayansi ya roboti, masuala ya ujenzi na uchanganuzi wa data, uchunguzi wa masuala mbalimbali ya kisayansi kwa kutumikisha teknolojia, sayansi za mawasiliano ya kiteknolojia, Tehama miongoni mwa kozi nyingine za kiteknolojia zitakuwa muhimu sana.

Kinavyotuagiza Kiswahili kuenda na uchao badala ya kuzama na uchwao, tuitumie fursa hii kuwaelekeza watoto wetu kuuona ulimwengu huku unakoelekea.

Vinginevyo tutajikuta katika jamii isiyo na ujuzi wa wenyeji bali inayotegemea ujuzi na maarifa kutoka kwa mataifa yaliyojipanga mapema. takribani kila sekta ya maisha imepiga hatua na sasa teknolojia ndiyo ramani inayoongoza hatua, safari na mikondo ya taaluma. Hapatakuwa na tasnia ya kitaaluma itakayokosa kuona umuhimu wa teknolojia katika ulimwengu wa sasa ila inayojizika.

Ilivyobainika katika kipindi hiki cha kupambana na korona, walimu pia watafundisha kwa mifumo ya kiteknolojia. Vyuo vyetu na taasisi za elimu havina budi kuchangamkia mabadiliko haya na kukita teknolojia katika kozi za mbinu za ufundishaji.

Serikali zetu nazo katika ngazi zake mbalimbali ziwekeze kikamilifu katika teknolojia ili mustakabali wa utendakazi uende na wakati. Bila wavuti au intaneti yenye uimara na ya bei nafuu hatutaweza kuyaendesha na kuyafanikisha haya. Tuwekeze katika vitu hivi muhimu na bila shaka kesho yetu itafana.

You can share this post!

KINA CHA FIKRA: Pambana na hali yako ili uiboreshe,...

GWIJI WA WIKI: Kennedy Opindi