Habari Mseto

Savula akamatwa kwa kukiuka masharti ya corona

July 7th, 2020 1 min read

BENSON AMADALA NA FAUSTINE NGILA

Mbunge wa Lugari Ayub Savula aliwalaumu polisi kwa kumdhulumu Jumapili asubuhi walipomtorosha kutoka kwa soko la Sabatia kaunti ndogo ya Butere.

Mbunge huyo alikamatwa akitia gari lake mafuta kwa kosa la kwa kutotii maagizo ya Wizara ya Afya ya kutoweka mikutano.

Hiyo ilitokea baada ya watu kukusanyika kwenye kituo hicho cha mafuta baada ya kumuona mbunge huyo aliyeandamana na kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula kwenye mkutano nyumbani kwa Mbunge wa Nambale John Bunyasi.

Bw Mudavadi na Bw Wetangula walikuwa washatangulia wakati wa tukio hilo.

Mbunge huyo alipelekwa kwenye kituo cha polisi cha Mumias na akaachiliwa baadaye.

Mbunge huyo alisema, “Nilikuwa nimesimama ili kuweka gari langu mafuta nikielekea Busia hapo ndipo umati wa watu uliokuwa sokoni uliniona na ukalizingira gari langu..

“Hata kabla nilipie mafuta polisi tayari walikuwa wamefika na kunilaumu kwa kuhutubia umati wa watu. Walisema nilikuwa nimekiuka mikakati iliyowekwa kudhibiti kusambaa kwa corona na wakaniuliza niandamane na wao hadi kituo cha polisi cha Mumias.”

Mbunge huyo alikaa kwenye kituo cha polisi kwa saa moja huku habari kuhusu kukamatwa kwake ziliposambaa. Wafuasi wake walikusanyika kwenye kituo hicho cha polisi na kuomba kuachiliwa kwake.