Michezo

Schmeichel aisaidia Leicester kukwepa kichapo

June 24th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIPA Kasper Schmeichel wa Leicester City alisalia kula na kushiba sifa kutoka kwa kocha wake Brendan Rodgers baada ya kuokoa penalti katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uliowashuhudia wakiambulia sare tasa dhidi ya Brighton mnamo Juni 23, 2020.

Schmeichel ambaye ni mzawa wa Denmark aliipangua penalti ya Neal Maupay ambaye aliingia katika mechi hiyo dhidi ya Leicester akiwa shujaa baada ya kuzamisha chombo cha Arsenal mwishoni mwa kipindi cha pili katika mechi ya awali.

“Kasper aliokoa penalti ambayo vinginevyo, ingeua kabisa ari yetu na kutikisa uhai wa matumaini yetu ya kukamilisha kampeni za muhula huu ndani ya mduara wa tatu-bora kileleni,” akatanguliza Rodgers ambaye ni kocha wa zamani wa Liverpool, Swansea City, Watford na Celtic.

“Hapana shaka kwamba ni miongoni mwa makipa bora zaidi kwa sasa katika kipute cha EPL. Ushawishi wake langoni na uongozi wake kikosini ni mambo yanayohisika sana,” akaongeza Rodgers kwa kusisitiza kwamba kipa wake huyo hutumia muda mwingi sana kutafiti jinsi wanasoka wengi wa EPL hupiga penalti zao.

“Schmeichel husoma mbinu zote za jinsi wanasoka mbalimbali wa kikosi pinzani hupiga penalti siku chache kabla ya mechi. Hilo humweka katika nafasi nzuri za kupangua baadhi ya mikwaju katika michuano muhimu,” akasema Rodgers.

Leicester kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 55, tisa zaidi kuliko Manchester United wanaokamata nafasi ya tano. Kwa upande wao, Brighton walisalia katika nafasi ya 15 kwa alama 33, sita zaidi kutoka kwenye mduara wa vikosi vinavyokodolea jicho hatari ya kushushwa daraja mwishoni mwa muhula huu.

Leicester kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Chelsea katika raundi ya sita ya Kombe la FA mnamo Juni 28 huku Brighton wakiwaalima Manchester United ligini mnamo Juni 30, 2020.