Sekta kuu ya bodaboda ilivyotekwa na wahalifu

Sekta kuu ya bodaboda ilivyotekwa na wahalifu

MARY WANGARI NA STEPHEN OKETCH

TUKIO la hivi majuzi ambapo wanamke mmoja alishambuliwa na kudhulumiwa kingono na waendeshaji bodaboda jijini Nairobi limeendelea kuibua hisia kali miongoni mwa Wakenya huku likianika uozo uliokithiri katika sekta hiyo.

Bodaboda ni sekta ndogo muhimu ya uchukuzi lakini ambayo imetekwa na wahuni. Wengi wa waendeshaji bodaboda hawajali sheria wala kuheshimu mamlaka. Wana ulimwengu wao, ambapo wao ndio sheria.

Afisa mkuu wa polisi Mwangi King’ori na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Julius Karangi ni mfano tu wa Wakenya walioonja hamaki na utundu wa magenge ya wanabodaboda.

Mnamo Agosti 2021, Bw King’ori alinusurika kichapo cha mbwa aliposhambuliwa na waendeshaji bodaboda baada ya kuhusika kwenye ajali katika eneo la Lang’ata, Nairobi.

Afisa mkuu huyo wa polisi ambaye sasa ahudumu katika Wizara ya Masuala ya Kigeni alilazimika kukimbilia usalama wake kutoka kwa kundi la bodaboda waliokuwa wakimpiga kabla ya kuokolewa na maafisa wa trafiki.

Kuna uwezekano mkubwa kwamba, Bw Kingori, kama afisa wa ngazi za juu katika idara ya polisi huenda alikuwa na silaha hatari ambayo pengine angelazimika kuitumia angehisi maisha yake yamo hatarini. Lakini hilo haliwatishi wanabodaboda.

Isitoshe, aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Jenerali (Mstaafu) Julius Karangi alinusurika kuteketezwa pamoja na gari lake baada ya kuhusika katika ajali mbaya mnamo Oktoba 31, 2020.

Bw Karangi alikuwa akielekea nyumbani kwake wakati mwendeshaji bodaboda aligonga gari lake nyuma na kumlazimu kushuka ili kulikagua. Aliokolewa na polisi waliokuwa karibu.

“Baada ya dakika chache tu, mamia ya waendeshaji bodaboda walikuwa wamefika. Walinizingira huku wakipiga honi na kutoa vitisho vya kila aina. Niliketi ndani ya gari langu kwa ujasiri. Ikiwa walijaribu kuniteketeza, ingekuwaje kama angekuwa mmoja wenu? Mngegeuzwa majivu ghafla na pengine kuteketeza gari vilevile,” alisema.

Jenerali huyo alisimulia haya alipokuwa akiwahutubia waombolezaji kwenye mazishi ya Mzee Stephen Mucheru Ngotho, 75, aliyeuawa na mwendeshaji bodaboda kwenye barabara ya Kutus-Kagio.

Mnamo Februari 17, genge la waendeshaji bodaboda lilishambulia na kuteketeza gari la Naibu Gavana Kaunti ya Kisii Joash Maangi kufuatia ajali iliyofanyika eneo la Olulung’a, Kaunti ya Narok.

Na hivyo ni sehemu ya visa vichache ambavyo vimeweza kuripotiwa. Ingawa sekta ya bodaboda inatekeleza wajibu muhimu nchini, ikiwemo kurahisisha usafiri katika sehemu za miji na mashinani na kutoa ajira kwa maelfu ya vijana, sasa imegeuzwa kuwa ya kihuni na inayosheheni wahalifu.

Wengine walionusurika kifo mikononi mwa magenge ya wanabodaboda wahuni pia wamevunja kimya chao na kujitokeza kusimulia masaibu ya kutisha waliyopitia.

Bw Charles Mwangi, 42, mwajiriwa wa Umoja wa Afrika, (AU) anashukuru kuwa hai baada ya kushambuliwa na genge la waendeshaji bodaboda mwezi uliopita, Februari 20.

Tukio hili lilimwacha mahututi na kumfanya alazwe katika hospitali ya Aga Khan, Nairobi kwa siku nne kwa gharama ya Sh327,000. Alikuwa akielekea nyumbani eneo la Garage, Kasarani, jijini Nairobi.

“Pikipiki iliyokuwa imebeba watu wawili iligonga gari langu. Nilitoka kuwajulia hali lakini kabla ya kufahamu kilichokuwa kikiendelea, niliona genge la waendeshaji bodaboda wakiwa wamenizunguka na kuanza kunivamia kwa mateke na mangumi. Kitu cha mwisho ninachokumbuka kabla ya kupoteza fahamu ni askari akiwatawanya.” “Tulikuwa tumelipwa na nilikuwa na Sh40,000 pesa taslimu kwenye gari walizochukua pamoja na nakala kadhaa za vitabu lakini kwa bahati nzuri hawakupata simu nilikokuwa nimeificha,” anasimulia.

Kinaya ni kuwa, abiria wawili wa pikipiki iliyohusika kwenye ‘ajali’ walikuwa miongoni mwa wahuni walioonekana na walioshuhudia kisa hicho wakichokora gari la Bw Mwangi kutafuta cha kuiba.

“Bodaboda ni genge linalopaswa kusambaratishwa wawe hai au wakiwa wamekufa. Uhuni na ukosefu wa nidhamu barabarani umeongezeka kupindukia. Mwendeshaji mmoja wa bodaboda alinisababisha kubingirika na gari langu nilipokuwa nikiepuka kumgonga alipoingia ghafla barabarani bila kutazama kwa makini. Hebu fikiria hata hakusimama!” aeleza Eddy Bwire.

Bila shaka huu ndio wakati mwafaka wa kutekeleza mapendekezo ya jopokazi lililoteuliwa na serikali kuangazia mazingira na utendakazi wa wahudumu wa bodaboda nchini.

You can share this post!

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Ukijiamini na uzingatie...

Ubabe wa Mvurya, Joho kuibuka upya

T L