Sekta ya afya pabaya maskini kwa matajiri wakiathirika

Sekta ya afya pabaya maskini kwa matajiri wakiathirika

Na CHARLES WASONGA

KUFELI kwa serikali kushughulikia changamoto zinazoathiri sekta ya afya kumechangia Wakenya wengi kufariki kutokana na maradhi ambayo yanaweza kutibiwa humu nchini kwa gharama ya chini.

Ukosefu wa dawa, vifaa vya matibabu na migomo ya kila mara ya wahudumu wa afya ni miongoni wa matatizo ambayo yanasibu sekta hii ambayo ni muhimu zaidi kwa ustawi wa nchi.

Hii ni kando na sakata ya mabilioni ya fedha ambayo imeathiri asasi muhimu kama vile Mamlaka ya Dawa (KEMSA).

Hali imekuwa mbaya zaidi kufuatia mlipuko wa janga la Covid-19 mapema mwaka 2020 ambapo serikali ilielekeza juhudi na rasilimali nyingi katika vita dhidi ya janga hilo na kutelekeza maradhi mengine, kama vile kansa.

Hii ni licha ya kwamba Afya Kwa Wote (UHC) ni mojawapo ya Ajenda Nne Kuu za Maendeleo ambazo serikali ya Jubilee imeazimia kutekeleza ifikapo mwaka wa 2022.

Utekelezaji wa mpango huo kwa njia ya majaribio katika kaunti za Kisumu, Isiolo, Machakos na Nyeri haujazaa matundo yoyote kwani idadi kubwa ya raia wamekuwa wakifariki kutokana na maradhi ya kawaida. Isitoshe, mpango huo haujatekelezwa katika kaunti zingine 43 alivyoahidi Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2018 Desemba alipoongoza uzinduzi wake mjini Kisumu.

Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU) Chibanzi Mwachonda juzi alinukuliwa akisema kuwa mpango wa UHC hauwezi kufaulu ikiwa serikali haiyapi kipaumbele masilahi ya wahudumu wa afya.

“Sisi kama wahudumu wa afya ndio kiungo muhimu zaidi katika kufanikishwa kwa mpango huo. Ikiwa masilahi yetu hayatashughulikiwa basi UHC itasalia kuwa ndoto. Wakenya hawanufaiki kutokana na mpango huo ikiwa wahudumu wa afya wataendelea kunyimwa haki yao kama vile marupurupu, bima ya matibabu na vifaa vya kazi,” akasema Dkt Mwachonda.

Madaktari, wauguzi, na wahudumu wengine wamekuwa wakigoma tangu mwaka jana wakidai walipwe marupurupu pamoja na mahitaji mengine wakati huu wa janga la corona.

Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF) nayo imefeli kwa kufeli kugharamia sehemu kubwa ya gharama ya magonjwa sugu kama vile corona na kansa. Hazina hiyo imekuwa ikilipia gharama ndogo zaidi huku wagonjwa wakilazimika kujazia gharamia nyinginezo.

Licha ya kwamba ni watu wa kawaida ndio huathirika zaidi kutokana na kufeli kwa sekta ya afya nchini, watu mashuhuri pia hawajasazwa.

Hii ni kufuatia vifo ambavyo vimekuwa vikitokea katika siku za hivi karibu na hivi punde kufariki akiwa ni Mbunge wa Juja Francis Munyao Waititu.

Marehemu Waititu ameongezeka katika orodha ya wabunge sita ambao wamefariki wakiwa afisini katika bunge 12.

Mbunge huyu maarufu kwa jina, Wakapee, alifariki katika hospitali ya MP Shah, Nairobi Jumatatu usiku ambako amekuwa akilazwa tangu Februari mwaka huu akiugua kansa ya ubongo.

Bw Waititu ameaga siku chache baada ya Mbunge wa Bonchari John Oroo Oyioka kufariki katika hospitali ya Aga Khan, Kisumu akiugua kiharusi.

Wengine ambao wamefariki tangu bunge la 12 lianze kazi ni; Justus Murunga (Matungu), James Lusweti Mukwe (Kabuchai), Suleiman Dori (Msambweni) na aliyekuwa Mbunge wa Kibra Ken Okoth (Kibra). Nao maseneta ambao wamefariki ni Boniface Kabaka na Yusufu Haji.

Magonjwa sugu kama saratani yameondokea kuwa chanzo cha vifo vya Wakenya haswa wale wenye mapato ya chini kutokana na gharama kuwa ya tiba.

Magonjwa hayo sugu husababishwa na mambo mengi ikiwemo kemikali ambayo hutumiwa kunyunyizia mazao shambani na bidhaa mbalimbali za tumbaku ambayo huruhusiwa kuingizwa nchini kiholela.

Majuzi ilifuchuka kuwa kampuni ya sigara, BAT, inaendelea kusambaza bidhaa kwa jina ‘Lyfy’ ambayo hutumiwa na vijana kama mbadala wa sigara.

Uchunguzi wa kisayansi umabaini kuwa bidhaa hii ina kemikali ya “nicotine” yenye madhara makubwa mwilini mwa mwanadamu. Hii ni licha ya kupigwa marufuku na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

Kulingana na takwimu kutoka kwa Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) karibu Wakenya 40,000 hupatikana kuugua kansa kila mwaka, huku karibu 15,000 miongoni wakiwa Wakenya wa kawaida wasio na uwezo kifedha.

Mwenyekiti wa Kenya Network of Cancer Organizations (KNCO) David Makumi anasema asilimia 75 ya wagonjwa wa kansa husaka matibabu mataifa ya nje kwa sababu serikali imefeli kuanzisha vituo vya tiba hiyo nchini.

“Hali hii imechangizwa ana usimamizi mbaya wa sekta ya afya na kukithiri kwa sakata za ufisadi. Zaidi ya Sh10 bilioni ambazo Wakenya hutumia kila mwaka kugharamia matibabu nje ni pesa nyingi ambazo zinaweza kutumiwa kuanzisha vituo vya kuwahudumia wagonjwa wa kansa nchini,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Mwilu alalamikia rundo la kesi kortini

Wito serikali isiingize nchi kwa madeni zaidi