Habari Mseto

Sekta ya chai kupigwa jekiseneti ikipitisha mswada

December 20th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la seneti Jumatatu litafanya kikao maalum kujadili Mswada mpya wa sekta ya Chai ambao unasheheni mapendekezo yatakayowasaidia wakulima wa zao kupata faida.

Kwa mfano, ukipitishwa na kutiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta usimamizi wa sekta ya chai utarejeshwa chini ya Bodi ya Chai Nchini (TBK) huku mamlaka mengi ya Shirika la Ustawi wa Chai Nchini (KTDA) yakitwaliwa na asasi hii mpya itakayosimamiwa na Serikali Kuu.

Kanuni mpya za uzalishaji na uuzaji zao hili pia zitaanza kutekelezwa kando na kuondolewa kwa ada nyingi ambayo KTDA imekuwa ikiwatoza wakulima.

Mfano ni Sh3 kwa kila kilo ya majani chai inayouzwa, ambazo hutozwa wakulima katika bonasi yao kila mwaka.Spika wa Seneti Kenneth Lusaka aliitisha kikao hicho maalum kufuatia ombi kutoka kwa Kiongozi wa Wengi Samuel Poghisio, lililoungwa mkono na maseneta 15.

“Kwa mujibu wa Katiba na sheria za bunge nimeitisha kikao maalum cha seneti Jumatatu, Desemba 24, 2020 kuanzia saa nane na nusu alasiri katika ukumbi wa mijadala katika seneti. Hii ni baada ya kuridhika kwamba taratibu zote zimefuatwa na kiongozi wa wengi aliyewasilisha ombi,” akasema kwenye ilani iliyochapishwa katika gazeti rasmi la serikali Desemba 18, 2020.

Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot ambaye ni mdhamini wa mswada huo alielezea matumaini kuwa maseneta watapitisha mswada huu ambao ulipitishwa katika bunge la kitaifa mnamo Desemba 3.

“Kesho (leo) kazi itakuwa rahisi kwetu kwa sababu wenzetu katika bunge la kitaifa hawakufanya mabadiliko makubwa katika mswada huu.Kimsingi, mapendekezo muhimu ambayo tulipendekeza yamedumishwa,” akasema.

Kwa mujibu wa mswada huo, pesa zitakazopatikana kutokana na mauzo ya zao hilo sasa hazitapelekwa kwa akaunti ya KTDA bali katika akaunti ya viwanda vya majani chai.

“Wakulima watapokea asilimia 50 ya mauzo ya zao hilo katika mnada baada ya fedha hizo kupokewa katika akaunti za viwanda huku fedha zilizosalia wakizipokea mwisho wa mwaka,” mswada huo unaeleza.

Vile vile, wakulima watapokea malipo hayo baada ya siku 14 tofauti na hali ilivyo sasa ambapo KTDA huchelewesha malipo hayo kwa hadi mwaka mmoja watakuwa wakipokea malipo hayo, kila mwezi, kutoka kwa viwanda vya majani chai katika maeneo yao.

Chini ya sheria hiyo TBK ndio imetwikwa wajibu wa kuunda kanuni za utawishaji, mnada na uuzaji zao hilo ng’ambo. Baadhi ya Kanuni hizo zilizinduliwa mwaka jana na Waziri wa Kilimo Peter Munya.