Makala

SEKTA YA ELIMU: Dhuluma kwa wanafunzi na matumizi ya mihadarati tishio kuu shule za upili

July 17th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

VISA vya mateso ya wanafunzi vilivyoripotiwa majuzi katika Shule za Upili za Nairobi School na Sawagongo ni kielelezo cha uozo wa kimaadili uliokithiri katika shule nyingi za upili humu nchini.

Ni uozo ambao unapasa kutafutiwa suluhisho la kudumu.

Inasikitisha kuwa wanaoendeleza dhuluma hizi ni viranja ambao wanapaswa kuwa katika mstari wa mbele kudumisha nidhamu shuleni. Katika shule ya Nairobi School, inaripotiwa kwamba mvulana wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 15 alipigwa na viranja kiasi cha kufanyiwa upasuaji wa ubongo.

Japo Waziri wa Elimu Profesa George Magoha ameagiza uchunguzi ufanywe ili kubaini chanzo cha visa hivi viwili, huenda uchunguzi huo usifichue ukweli wowote kwa sababu tayari wasimamizi wa shule hizo wamewatetea viranja hata kabla ya uchunguzi kuanza.

Hii ina maana kuwa wasimamizi hao, hasusan walimu wakuu, hawatatoa habari muhimu kwa maafisa wa Wizara ya Elimu watakaoendesha uchunguzi huo kwa sababu wanafahamu fika kwamba wao ndio hatimaye wataelekezewa lawama.

Ifahamike kuwa visa vilivyoripotiwa majuzi si vya kwanza wala vya mwisho. Kwa miaka kadha, wanafunzi wa vidato vya kwanza wamekuwa wakidhulumiwa si tu na viranja bali hata wenzao wa madarasa ya juu.

Kwa mfano, mnamo 2017, ripoti za wanafunzi wa kidato cha kwanza kutendewa ukatili ziliibua kero miongoni mwa wazazi wa Shule ya Upili ya Alliance na Wakenya kwa ujumla, hali iliyochangia kustaafishwa mapema kwa aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, David Kariuki.

Hii ni baada ya uchunguzi ulioendeshwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) pamoja na Wizara ya Elimu kuelekeza kidole cha lawama kwa usimamizi wa shule.

Kwa mfano, ilibainika kuwa viranja walitwikwa mamlaka mengi kiasi kwamba baadhi yao walijihisi kuwa “miungu” wa kuabudiwa.

Kwa hivyo, ni wazi kuwa walimu wakuu wanapaswa kuwadhibiti viranja na wanafunzi wengine watundu wenye tabia ya kuwatesa wenzao ikizingatiwa kuwa ukatili kama huu huathiri mwanafunzi hata baada ya kukamilisha masomo yake.

Uabudu shetani

Wadau wanasema mbali na dhuluma kwa wanafunzi, matumizi ya dawa za kulevya na pombe pamoja na uabudu wa shetani ni miongoni mwa maovu ambayo yamekithiri katika shule nyingi za humu nchini.

“Kwa hakika, takriban asilimia 70 ya shule zote za upili humu nchini zimeathiriwa na visa vya utovu wa nidhamu, kama vile mateso ya wanafunzi na matumizi ya mihadarati. Uabudu wa shetani na ngono za mapema pia ni kero kuu,” anasema mwalimu mmoja wa shule ya upili ambaye aliomba tulibane jina lake.

Kauli ya mwalimu huyu imethibitishwa na yaliyomo kwenye ripoti ya hivi punde iliyotolewa na Halmashauri ya Kupambana na Vileo Haramu na Mihadarati (Nacada) kuhusu kero ya matumizi ya dawa za kulevya katika shule za upili za humu nchini.

Ripoti hii iliyotayarishwa baada ya uchunguzi uliofanywa katika shule za umma kote nchini kuanzia Oktoba mwaka jana, imefichua kuwa wanafunzi huingilia uraibu wa kutumia dawa za kulevya na vileo wakiwa na umri wa kati ya miaka 13 na 15.

Ilibainika kuwa wanafunzi hutumia dawa kama vile, bangi, Cocaine, mandrax, miraa, pombe na sigara huku shule za maeneo ya Kati na Mashariki ya nchi zikiathiriwa zaidi.

“Wanafunzi wengi huanza kutumia mihadarati na pombe wakiwa na umri wa kati ya miaka 13 na 15. Hii ina maa na kuwa wanafunzi hukumbatia tabia hii wakiwa katika kidato cha kwanza na pili,” inasema ripoti hiyo.

Jumla ya wanafunzi 3,908 walihojiwa katika utafiti huo ambapo asilimia 70 kati yao walikuwa wavulana huku asilimia 30 wakiwa wasichana.