Makala

SEKTA YA ELIMU: Magoha akome kutoa maagizo tu, amalize utovu wa nidhamu shuleni

June 26th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

VISA vya utovu wa nidhamu vimeanza kushuhudiwa katika shule za upili kwa mara nyingine katika muhula huu kisa cha hivi punde kikitokea katika shule ya upili ya Uriri, iliyoko kaunti ya Migori.

Lakini inachoshangaza kwamba wizara ya elimu haionekani kuwa makini kuzima visa kama hivyo ambavyo husababisha hasara ya pesa nyingi.

Mnamo Jumatatu, Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha, aliwataka wakurugenzi wa elimu katika ngazi za kimaeneo na kaunti kufuatilia kwa karibu yale yanayoendelea katika shule za upili zilizoko katika maeneo wanakosimamia.

Profesa Magoha aliwataka maafisa hao kukagua shule hizo angalau mara moja kila baada ya majuma mawili.

“Hatutaki kusikia shule zinateketezwa wakati huu ambapo wanafunzi, haswa wale wa kidato cha nne kuwa wanajiandaa kwa mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne,” akasema alipoongoza mkutano wa wadau kupanga mikakati ya kuzima udanganyifu katika mtihani wa mwaka huu.

Inashangaza kuwa waziri hakutoa ushauri au mwelekeo wowote kwa walimu wakuu ambao wasimamizi wa karibu shuleni.

Kwa mfano, inadaiwa kuwa vurugu zilizotokea katika wiki hii katika shule ya upili ya Uriri ilitokana na kero la wanafunzi baada ya usimamizi wa shule kuwanyima nafasi ya kutazama mechi ya kandanda kati ya Kenya na Algeria.

Na bila shaka amri kama hiyo hutolewa na mwalimu mkuu.

Itakumbukuwa kuwa kumekuwa na ongezeko la visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi katika shule za upili tangu mwaka wa 2016 katika muhula huu wa pili lakini wizara ya elimu haijaweza kuchukua hatua zozote madhubuti za kivizima.

Kwa mfano, katika mwaka huo, masomo yalivurugika katika takriban shule 107 baada ya wanafunzi kuteketeza majengo kadha, haswa mabweni.

Na mwaka jana zaidi ya shule 10 za upili zilifungwa katika muhula wa pili baada ya wanafunzi kuzua vurugu na kuharibu mali ya shule.

Kuiziba mianya

Kulingana na ripoti moja iliyoandaliwa na Wizara ya Elimu, baadhi ya wanafunzi hugoma katika mihula ya pili hofu ya kuanguka mtihani kufuatia hatua ya wizara hiyo kuziba mianya yote ya udanganyifu katika mtihani huo.

Kando na hofu ya mitihani, haswa ule wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE), ripoti hiyo ilitaja utepetevu wa wasimamizi wa shule, na matumizi ya mihadarati miongoni mwa baadhi kama vichochezi vingine vya machafuko shule.

Kwa mfano, ilidaiwa kuwa baadhi ya wanachama wa bodi ya usimamizi wa shule ya moja katika kaunti ya Meru walichochea fujo za wanafunzi mwaka jana kama hatua ya kumwadhibu mwalimu mkuu ambaye hawakuelewana naye kuhusu masuala ya fedha.

Hata hivyo, katika mapendekezo yake jopo kazi lililoongozwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kati Bi Claire Omollo na kuchunguza chimbuko la migomo shuleni mnamo 2016 liliitaka Wizara ya Elimu kuimarisha usalama katika shule haswa zile za mabweni.

Aidha, wanachama wa jopo kazi hilo walipendekeza kuwa hatua za kimakusudi zichukuliwe kuimarisha vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa wanafunzi, walioyatambua tatizo kuu.

Kwa msingi huu, ni muhimu kwa wasimamishi wa shule za upili za mabweni kuwa waangalifu katika muhula huu wa upili ili kusitokee ghasia zitakazovuruga masomo.

Na waziri Magoha anapaswa kuhakikisha lengo hili linafikiwa.