Makala

SEKTA YA ELIMU: Mikakati ya kuzima wizi wa mitihani ni ya kupongezwa

October 16th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HUKU mitihani ya kitaifa inapokaribia kuanza suala kuu ambalo Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC), Wizara ya Elimu na ile ya Usalama wa Ndani huzingatia kwa uzito ni kuzima mianya inayoweza kufanikisha udanganyifu.

Na serikali hutumia rasilimali nyingi kuzima uovu huu kwa sababu chini ya mfumo wa sasa wa elimu, mitihani hii ndio hutumiwa kama nyenzo au ngazi ya kumvukisha mwanafunzi kutoka daraja moja hadi lingine, kimasomo.

Mtihani wa kitaifa wa darasa nane (KCPE) hutumiwa kuchuja wanafunzi watakaojiunga na shule za upili za viwango vya kiwilaya, kikaunti au kitaifa. Na mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) ni “kichungi” cha kubaini wanafunzi watakaojiunga na vyuo vikuu, vyuo vya kadiri na vyuo vinginevyo kwa masomo ya juu.

Kwa hivyo, udanganyifu katika mtihani katika mtihani wa KCPE huchochewa na hamu ya wahusika kujiunga na shule bora za upili hasa, zile za kitaifa kwa matumaini kuwa wataweza kufaulu kupata alama nzuri mtihani wa KCSE na hatimaye kujiunga na vyuo vikuu. Katika vyuo vikuu wanafunzi hawa hutaraji kwamba watafanya kazi bora ambazo zitawawezesha kupata ajira na kuishi maisha nzuri.

Dhana kama hii ni potovu kwani imebainika kuwa visa vya udanganyifu hushusha hadhi ya mitihani ya kitaifa, viwango vya elimu nchini na kuathiri maisha ya baadaye ya wanafunzi walifaidi kwayo.

Kwa mfano, imebainika kuwa baadhi ya wanafunzi waliopata alama za juu mitihani ya KCSE kwa udanganyifu na kuitwa kusomea kozi kama udaktari au uhandisi katika vyuo vikuu huishia kulemewa na kuomba wasajiliwe kwa kozi zingine “nyepesi”. Aidha, wengine hujiondoa na kuamua kujiunga na vyuo vya kadri kusomea kozi nyinginezo wanazoweza kumudu.

Hii ndio maana Chama cha Kitaifa cha Wazazi (KPA) kimechangamkia mikakati ambayo KNEC, Wizara ya Elimu na Serikali kwa jumla iweka kuzima visa vya undanganyifu katika mitihani ya kitaifa ya KCPE na KCSE mwaka 2019.

“Sisi kama wazazi tunafurahia mikakati iliyowekwa na serikali kuzuia wizi au udanganyifu wa aina yoyote katika mitihani ijayo ya kitaifa. Tunatumai kuwa matokeo ya wanafunzi hayatafutiliwa mbali kwa sababu kubainika kuwa walishiriki udanganyifu,” akasema mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho Nicholas Maiyo.

KCPE inatarajiwa kuanza Oktoba 28 hadi Oktoba 31 huku KCSE ikianza Novemba 4 hadi Novemba 27.

Jumla ya watahiniwa 1,089,671 wanatarajiwa kufanya KCPE na wengine 698,935 watafanya KCSE katika vituo mbalimbali kote nchini.

Mnamo Jumatatu Waziri wa Elimu Profesa George Magoha na mwenzake wa Usalama Dkt Fred Matiang’i walitoa hakikisho kwamba mikakati tosha imewekwa kuzuia udanganyifu katika mitihani hiyo. Walionya kwamba mtu yeyote atakayepatika akijaribu kusaidia undanganyifu.

“Maafisa wa Knec, walimu au maafisa wa usalama ambao watawasaidia watahiniwa kupata habari zozote kuhusu mitihani kabla ya wakati wa mtihani wataadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh2 milioni au kifungo kisichozidi miaka 10 gerezani au adhabu zote mbili,” akasema Waziri Matiang’i katika mkutano wa kujadili namna ya kuendesha mitihani, uliofanyika katika Chuo cha Masuala ya Serikali (KSG), Nairobi.

Alisema konteina 479 zitatumika kuhifadhi karatasi za mitihani katika kaunti ndogo 338 kote nchini.

“Polisi watano watalinda kila konteina. Watasimamiwa na afisa mmoja ambaye atakuwa akitoa habari kwa wakuu wa usalama katika kaunti kuhusu usalama wa konteina hizo,’ akasema Waziri Matiang’i.