Makala

SEKTA YA ELIMU: Miundomsingi katika shule za walemavu pia inafaa ikaguliwe

October 2nd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MNAMO Jumatatu wiki hii Naibu Gavana wa Nyeri Caroline Karuga alitamaushwa na changamoto zinazowakabili wanafunzi wanaoishi na aina mbalimbali za ulemavu nchini.

Alikuwa akiongoza halfa ya uzinduzi wa mpango wa kuwasaidia wanafunzi wenye changamoto hizi kupata elimu katika kaunti hiyo kwa mpango maarufu kama, “Wezesha Elimu Programme”.

Alisema: “Nilitembelea shule moja ya watoto hawa nikapandwa na hisia za huruma nilipowaona wanafunzi hao ambao hawana uwezo wa kutembea, wakitambaa kuenda kwenye bafu. Kwa hivyo, naiomba Wizara ya Elimu kufanya ukaguzi wa shule hizo kwani nyingi hazina miundomsingi faafu kwa wanafunzi walemavu.”

Kauli ya naibu huyo wa Gavana inaakisi baadhi ya changamoto zinazozikabili shule maalum za wanafunzi wenye ulemavu nchini ambazo hukidhi mahitaji ya takriban wanafunzi 125,000.

Kulingana na ripoti iliyotayarishwa mwaka jana na Wizara ya Elimu kwa ushirikiano na Taasisi ya Elimu Maalum Nchini (KISE), shule nyingi za watoto wanaoishi na ulemavu zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa miundo msingi maalum na vifaa hitajika vya masomo.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa shule nyingi za aina hii bado hazina madarasa, mabweni na vyoo vilivyojengwa mahsusi kwa matumizi ya wanafunzi wenye ulemavu. Ilibainika kwamba katika baadhi ya shule, miundo msingi iliyojengwa zamani haijafanyiwa ukarabati ili kuafiki mwongozo maalum uliotolewa na Wizara ya Elimu kuhusu muundo hitajika wa majengo kama hayo.

“Baadhi ya mabweni hayajajengwa kwa kuzingatia kanuni maalumu kuhusu usalama,” inasema ripoti hiyo.

Ripoti hiyo kwa jina “Report on National Survey on Children with Disabilitity and Special Need in Education” iliyozinduliwa mnamo Novemba 28, 2018 ni zao la utafiti uliofanywa katika baadhi ya shule maalum katika maeneo mbalimbali nchini mnamo 2017.

Idadi ya wanafunzi

Katika Shule ya Upili ya Joytown iliyoko Thika Mjini yenye wanafunzi 292, ilibainika kuwa mabweni yana wanafunzi wengi kupita kiasi.

Kwa hivyo, baadhi yao wanalazimika kutumia vitanda virefu aina ya double-decker ilhali wengi wao wamelamaa miguu na hutumia viti vya magurudumu na mikongojo.

Baadhi ya madarasa hayakuwa na miundo msingi ya kuwasaidia wanafunzi kuingia kwa urahisi “ramp” na madawati ya maalumu kwa matumizi hususan ya wafunzi waliolemaa miguu na mikono.

Na katika shule nyingine iliyoko Murang’a, ilibainika kuwa baadhi ya madirisha ya mabweni yaliwekwa juu kiasi kwamba ni vigumu kwa wanafunzi kuyafungua kwani yamechomelewa vyuma kwa upande wa nje.

Hali hii ni kinyume na mwongozo kuhusu usalama, unaohitaji kwamba madirisha yajengwe kwa namna ambayo yanaweza kufunguliwa na wanafunzi kwa urahisi na yasiwe na vizuizi vyovyote.

“Japo serikali inaendesha kampeni ya uhamasisho kuhusu haja ya wazazi kuhakikisha watoto walemavu wanapelekwa shuleni, kinaya ni kwamba serikali haijatoa rasilimali za kutosha kukidhi mahitaji ya watoto walemavu,” anasema Bw Raphael Aura, mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule zinazotoa Mafunzo Maalum (Kenya Special Schools Principals Association-KSSPA).

Anapendekeza kwamba ukaguzi ambao unaendeshwa sasa na serikali kubaini shule zenye majengo mabovu katika shule za msingi na za upili uendeshwe pia katika shule za wanafunzi wenye mahitaji maalum.