Makala

SEKTA YA ELIMU: Mpango wa elimu ya upili kwa wote utekelezwe kwa tahadhari

March 20th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WIKI jana Rais Uhuru Kenyatta alisema kwamba maafisa wa wizara ya elimu wamekuwa wakitembelea shule za upili za humu nchini kubaini zile ambazo zinahitaji upanuzi wa miundo mbinu kutokana na ongezo la idadi ya wanafunzi.

Akiongea katika shule ya upili ya Mang’u, kiongozi wa taifa alifichua kuwa ni baada ya shughuli hiyo kukamilika ambapo serikali itatoa fedha za kufadhili ujenzi wa madarasa na majengo mengine katika shule hizo.

“Wakati huu lengo letu ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofanya mtihani wa KCPE wanajiunga na shule za upili hata iwapo watakuwa wakisomea chini ya miti,” akasema Rais Kenyatta.

Lakini kauli ya Rais hailandani na ile iliyotolewa na Katibu wa Elimu Belio Kipsang’ mwaka jana kwamba tayari serikali ilikuwa imetenga Sh7 bilioni kufadhili mpango huo kama sehemu ya maandalizi ya mpango wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanapata nafasi katika shule hizo.

Rais Uhuru Kenyatta akisemezana na Kiranja Mkuu wa Mang’u High, Kitagwa Powell kwenye hafla ya utoaji zawadi shuleni humo Machi 16, 2019. Picha/ Samuel Miring’u

Wakati huu shule hizo zinakabiliwa na msongamano huku katika baadhi ya shule mwalimu mmoja akisomesha jumla ya wanafunzi 80 katika darasa moja.

Na katika baadhi ya shule za upili za mabweni, usalama wa wanafunzi unatiliwa shaka kutokana na msongamano katika vyumba vya malazi.

Swali ni je, kati ya Rais Kenyatta na Dkt Kipsang’ ni nani anasema ukweli kuhusu mikakati ya kukabiliana na kero hii?

Kauli hizi zinawakanganya wadau katika sekta ya elimu na kuibua wasiwasi wa viwango vya elimu kuendelea kudorora katika shule za umma.

Akiongea na safu hii, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu Nchini (Knut) Bw Wilson Sossion alisema kwamba hatua ya kwanza ni kwa serikali kuwaajiri walimu zaidi mbali na kujenga madarasa zaidi.

“Kwa sasa kuna uhaba wa walimu 87,489 katika shule zote za umma nchini. Shule za upili zinahitaji walimu 47,576 ilhali zile za msingi zina upungufu wa walimu 39,913. Serikali inafaa kuajiri walimu kwanza kabla ya kuanza mradi wa miundo msingi shuleni,” akasema katika mahojiano kwa njia ya simu.

Walimu kuajiriwa

Katibu huyo anaungama kuwa sera ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wa Msingi wanajiunga na shule za upili ni nzuri lakini serikali inapaswa kuhakikisha kuwa walimu wanaajiriwa kila mwaka.

“Hilo lisipofanyika bila shaka viwango vya elimu vitashuka na ni wananchi masikini ndio wataumia kwa sababu hawana pesa za kuhamishia watoto wao hadi shule za kibinafsi,” akasema Bw Sossion ambaye pia ni Mbunge maalumu.

Mapema mwaka 2019 Tume ya Huduma kwa Walimu Nchini (TSC) ilitangaza kwamba itaajiri walimu 5,000 katika shule za upili, idadi ambayo Bw Sossion anasema ni sawa na tone la maji katika bahari.

Mtaalamu wa masuala ya Elimu Dkt John Mugo anaunga mkono kauli ya Bw Sossion akisema kwamba kuajiri walimu zaidi kutaimarisha viwango vya masomo katika shule hizo chini ya mpango huu.

“Serikali inafaa kuzuia hali iliyoshuhudiwa nchini mnamo mwaka wa 2003 wakati utawala wa Rais mstaafu Mwai Kibaki ulianza kutekeleza mpango wa elimu ya msingi bila malipo. Viwango vya masomo vilishuka kutokana na ongezeko la idadi ya wanafunzi,” anasema mtaalamu huyu ambaye pia ni mkurugenzi wa mipango katika shirika la Twaweza East Africa.