Makala

SEKTA YA ELIMU: Nani atawaokoa wazazi dhidi ya kupunjwa kwa karo hizi za ziada?

January 8th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

IMEBAINIKA kuwa wafanyabiashara, walimu wakuu, wanachama wa bodi za usimamizi za shule na baadhi ya wawakilishi wa wazazi katika bodi hizo hushiriki njama ya kuwapunja wazazi kwa kuwaongezea mzigo wa karo.

Hii ndio maana shule zilipofunguliwa kwa muhula wa kwanza wiki hii wazazi walilalamikia hatua ya wasimamizi wa shule za upili kuwaongezea ada nyingi za ziada kando na viwango vya karo vilivyoidhinishwa chini ya mwongozo uliotolewa na Wizara ya Elimu.

Kulingana na mwongozo wa karo wa mwaka huu, wazazi wenye watoto katika shule za mabweni za ngazi ya kitaifa na kimkoa wanapaswa kulipa karo ya Sh53,554, kwa mwaka huku wale wa shule za kaunti na wilaya wanahitajika kulipa Sh40,545.

Na wazazi ambao watoto wao husomea katika shule za kutwa huhitajika kulipa Sh9,000 pekee za kugharimia chakula cha mchana. Hii ni kwa sababu serikali italipa Sh22,244 kama karo ya mafunzo kwa wanafunzi wote katika shule za mabweni na zile za kutwa.

Lakini kando na viwango hivi vya karo, uchunguzi umebaini kuwa wazazi wanaitishwa karo za ziada za kugharimia ujenzi wa miundo msingi, mishahara ya walimu walioajiriwa na bodi simamizi (BoMs) na ada ya kugharamia uharibu (caution fee), hata kwa wanafunzi wa zamani.

Kwa mfano, katika shule moja ya upili iliyoko kaunti ya Nairobi, kando na Sh53,554, wazazi wanahitajika kulipa Sh10,000 za ujenzi wa miundo Sh8, 000 za kuajiri walimu vibarua.

Na katika baadhi ya shule wazazi walilalamika kwamba walimu wakuu wanawalazimu kulipa takriban Sh7,000 za sare za shule ilhali mavazi hayo yanaweza kupatikana kwa bei ya chini katika maduka ya sare za shule.

“Shule imesisitiza kuwa sharti tulipe Sh7,000 za kugharImia sare ambazo tunaweza kupata katika maduka mengine kwa Sh3,000. Mwaka jana tuliitishwa Sh6,500 lakini mavazi hayo yakageuka kuwa ya thamani ya chini,” anasema mzazi mmoja ambaye ana watoto wawili katika shule moja ya upili katika kaunti ya Nairobi.

Na baadhi ya shule, hasa zile za mashambani, zimekuwa zikiwaagiza wazazi kununua sare na mahitaji mengine kutoka maduka mahsusi wala sio maduka mengine. Wazazi wanashuku kuwa huenda usimamizi wa shule husika zina uhusiano fulani za kibiashara na wenye maduka hayo kwa lengo la kuwapunja ikizingatiwa kuwa maduka hayo huwatoza bei ya juu.

Mwenyekiti wa Chama cha Wazazi Nchini (KPA) Nicholas Maiyo anasema wazazi wanafaa kuruhusiwa kununua sare na mahitaji mengine, katika soko huru.

“Wazazi wanakabiliwa na hali ngumu kiuchumi na hawafai kunyanyaswa katika hali hii. Wazazi waruhusiwe kununua mahitaji ya shule katika maduka yanayotaka mradi wahakikishe ni yenye thamani hitajika,” anasema.

Kuhusu karo za ziada, Bw Maiyo anaelekeza kidole cha lawama kwa wawakilishi wa wazazi katika BoMs ambao anasema hushawishika kwa njia fulani ili “kuwasaliti” wazazi wenzao kuwakubalia nyongeza ya karo.

“Baadhi ya walimu wakuu na wasimamizi wengine wamebuni mwenendo mbaya wa kutia mfukoni wawakilishi wa wazazi katika bodi simamizi na hivyo kupata nafasi ya kuongeza karo kiholela. Nataka Waziri wa Elimu George Magoha kuingilia kati suala hili,” akasema Bw Maiyo.

Kulingana na sheria, nyongeza yoyote ya karo au ada inapasa kuidhinishwa katika mkutano wa wazazi wa shule husika. Aidha, mkurugenzi wa elimu katika kaunti ndogo anafaa kufahamishwa kuhusu hatua hiyo kupitia kumbukumbu za mkutano wazazi ulioidhinisha nyongeza hiyo.