Makala

SEKTA YA ELIMU: Serikali iongeze ufadhili na usambazaji wa sodo shuleni

September 18th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

NI ukweli usiopingika kwamba usafi wa mwili ni ufunguo wa afya nzuri ya mwili na akili.

Utafiti umebaini kuwa wanafunzi ambao hawadumishi usafi wa mwili hufanya vibaya masomoni ikilinganishwa na wale ambao hudumisha usafi wa mwili nyakati zote.

Inasikitikisha kuwa licha ya serikali kufahamu ukweli huu, inazembea kutekeleza hatua za kuimarisha usafi haswa miongoni mwa wanafunzi wa kike.

Wiki jana taifa zima lilipokea kwa mshangao mkubwa habari kuhusu kifo cha msichana ambaye aliamua kujitoa uhai baada ya kuaibishwa na mwalimu wake shuleni. Kisa na maana, alichafua sare zake kwa damu ya hedhi.

Duru zilisema kuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mwanafunzi huyu wa darasa la sita katika shule ya msingi ya Kabiangek iliyoko eneobunge la Konoin, Kaunti ya Bomet kupata hedhi, hali iliyompata kwa mshtuko.

Kinaya ni kwamba ni mwalimu wa kike ndiye alimwaibisha marehemu badala ya kumpa ushauri na mwelekeo kuhusu namna ya kushughulikia tukio hilo la kimaumbile.

Lakini inasikitisha kuwa mkasa huo uliotokea wakati ambapo kwa muda wa mwaka mmoja, serikali imefeli kusambaza sodo katika shule za msingi na upili licha ya kuwepo kwa sheria inayoilazimu kufanya hivyo.

Inadaiwa kuwa hali hii imetokana na mvutano kati ya wizara ya Utumishi wa Umma na Masuala ya Jinsia na ile ya Elimu, kuhusu ni ipi inapasa kusimamia mpango huo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Elimu ya Msingi ya 2017, iliyofanyiwa marekebisho, wanafunzi wote wa kike walio katika umri wa kubaleghe wanapasa kupewa sodo bila malipo katika shule zote za umma; msingi na upili.

Sheria hii ni zao la mswada uliodhaminiwa na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Baringo Bi Grace Kiptui katika bunge la 11.

Mswada huo ulipitishwa katika bunge la kitaifa na kutiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Juni 21, 2017.

Hii ina maana kuwa kuanzia mwaka wa kifedha wa 2017/2018 Waziri wa Fedha amekuwa akitenga fedha katika bajeti ya kitaifa kwa ajili ya kugharimia mpango huo muhimu.

Kwa mfano katika mwaka wa kifedha wa 2018/2019 mpango huo ulitengewa Sh400 milioni na katika mwaka wa sasa, 2019/2020, mgao huo ulioongezwa hadi Sh460 milioni.

Hii ina maana kuwa wasichana waliofaidi kwa sodo mwaka jana na mwaka huu walipasa kupokea vifurushi vinne pekee kila mmoja kwa mwaka mzima.

Sababu ni kwamba kuna takriban wasichana 4.2 milioni waliotimu umri wa kubaleghe katika shule za umma za msingi na upili nchini.

Hii ina maana kuwa ufadhili huo hautoshi na shule nyingi haswa zile za mashambani, kama vile Kibiangek alikokuwa akisoma marehemu Chepngeno zisingesaidika.

Takwimu

Kulingana na takwimu kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), mmoja kati ya wasichana 10, waliobaleghe, katika mataifa yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara hukosa kuhudhuria vipindi shuleni wanapopata hedhi kwa kukosa sodo.

Hii ina maana kuwa wao hupoteza asilimia 20 ya saa zao za masomo hali ambayo huchangia wao kufanya vibaya katika mitihani ya kitaifa.

Nchini Kenya, inakadiriwa kuwa wanafunzi wanne wa kike, wenye umri kati ya miaka 14 na 18 wanatoka katika familia ambazo haziwezi kugharimia sodo.

Na wengi wa wanafunzi hawa hulazimika kukatiza masomo.

Kwa hivyo, kutokana na mkasa uliotokea majuzi, serikali inapasa kuamka na kulainisha mpango wa utoaji sodo bila malipo katika shule za umma.

Aidha, ufadhili kwa mpango huu pia unapasa kuongezwa.