Makala

SEKTA YA ELIMU: Tangazo la Magoha kuhusu karo halina mantiki na litawaumiza wazazi

December 4th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HATUA ya serikali kuwaruhusu walimu wakuu kuongeza karo katika shule za upili ili kupata fedha za kufadhili ujenzi wa miundo msingi imeibua maswali kuhusu uhalali wa ahadi yake kwamba imetenga Sh8 bilioni kwa shughuli hiyo.

Nao wazazi sasa wameingiwa na hofu kwamba huenda baadhi ya walimu wakatumia tangazo hilo la Waziri wa Elimu George Magoha kama mwanya wa kuwatoza karo za juu kupita kiasi.

Ndiposa Chama cha Kitaifa cha Wazazi (KNPA) kinaitaka Wizara ya Elimu kuweka viwango vya nyongeza ambavyo walimu wakuu wanapasa kuongeza na namna nyongeza hiyo itakadiriwa.

Mwenyekiti wa chama hicho Nicholas Maiyo ameelezea hofu kwamba tangazo hilo lililotolewa Jumatatu huenda likawapa ‘leseni’ wasimamizi wa shule kuwapunja “kwa kuongeza karo kiholela”.

“Kutangaza kwamba walimu watakuwa huru kuongeza karo ili kupatikane pesa za kujenga madarasa na majengo mengi shuleni hakutoshi. Waziri Magoha anafaa kutoa mwongozo kuhusu nyongeza hiyo ikizingatiwa kuwa shule za upili zina mahitaji tofauti. Vile vile, baadhi ya wasimamizi wa shule watawanyanyasa wazazi kwa kuwaongezea karo bila mpango wowote” Bw Maiyo anasema.

Anasema licha ya Waziri Magoha kufafanua kuwa sharti walimu wakuu wawaruhusu wazazi kuamua kiasi cha pesa zaidi ambazo watalipa hilo halitawezekana. “Wazazi sio wataalamu wa kukadiria thamani ya ujenzi wa darasa au bweni. Kwa hivyo, pendekezo la Profesa Magoha halina mantiki yoyote,” anasema Bw Maiyo.

Itakumbukwa kwamba mnamo Novemba 18, mwaka huu akihutubu wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) Profesa Magoha alisema kuwa serikali imetenga Sh8 bilioni za kufadhili mpango wa upanuzi wa miundo msingi katika shule za upili.

Alisema pesa hizo zitatumiwa kujenga madarasa zaidi, na majengo mengineyo, katika shule hizo ambazo zimeshuhudia ongezeko la wanafunzi tangu mwaka jana serikali ilipoanza kutekeleza sera ya kusajili asilimia 100 ya watahiniwa wa KCPE katika shule za upili.

Sasa swali ni je, mbona Waziri Magoha anabadili kauli na kuwatwika wazazi mzigo wa kufadhili ujenzi wa miundo msingi shuleni?

Kulingana na mtaalamu wa masuala ya elimu Emmanuel Manyasa, tangazo la Waziri Magoha kwamba walimu wakuu wanaweza kutoza karo zaidi kwa ajili ya kupata fedha za kufadhili ujenzi wa miundo msingi ni sawa na serikali kuungama kuwa ilianzisha sera ya kuwavukisha wanafunzi wote hadi shule za upili bila kufanya maandalizi.

“Hatua hii ya kuwabebesha wazazi mzigo wa ujenzi wa madarasa, vyumba vya malazi na miundo msingi mingine muhimu shule inaonyesha kuwa serikali haikuwa tayari kwa mpango huu. Serikali ilipasa kupanua shule za upili za umma kwanza kabla ya kuanzisha utekelezaji wa sera hii ya kuhakikisha kuwa watahiniwa wote wa KCPE wanajiunga na kidato cha kwanza,” anasema Bw Manyasa ambaye ni mkurugenzi mkuu wa Shirika la Uwezo Kenya ukanda wa Afrika Mashariki.

Kulingana na mwongozo wa karo unaotumika sasa, shule za upili za kitaifa hutoza karo ya Sh75,798 kila mwaka. Na baada ya serikali kulipa Sh22,244, wazazi huhitajika kulipa Sh53,554. Na shule za ngazi ya kaunti hutoza karo ya Sh62, 679 kila mwaka ambapo wazazi hulipa 40,535 huku shule za kutwa zikihitaji kutoza karo ya Sh9,000 pekee kila mwaka.

Lakini Bw Maiyo sasa anabashiri kwamba huenda baadhi ya shule za upili zikaongeza karo hadi kufikia kati ya Sh100,000 kwa misingi ya sababu iliyotolewa na Waziri Magoha endapo serikali haitatoa mwongozo kuhusu nyongeza hiyo.