Makala

SEKTA YA ELIMU: Uhamisho wa walimu utavuruga masomo Kaskazini Mashariki

February 5th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

INGAWA walimu ni afueni kwa walimu wasio wenyeji katika kaunti za Kaskazini Mashariki mwa Kenya baada ya Tume ya Huduma za Walimu (TSC) kukubali kuwapa uhamisho kutoka shule za maeneo haYo kwa sababu za kiusalama, wanafunzi katika maeneo hayo watapoteza pakubwa kimasomo.

Hii ni kwa sababu mipango mingi inayotekelezwa na serikali kupitia wizara ya elimu, mathalan, utekelezaji wa mtaala mpya wa umilisi na utendaji (CBC) na ule wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofanya mtihani wa darasa la nane (KCPE) wanajiunga na shule za upili, itaathirika.

Isitoshe, hatua hii itazidisha kero la uhaba wa walimu katika shule za umma eneo hilo, ambako kwa ujumla zina uhaba wa takriban walimu 28,000.

Mnamo Jumatatu wiki hii walimu hao ambao walipewa barua za uhamisho kutoka shule ambako wamekuwa wakifunza katika kaunti ya Garissa hadi shule za maeneo mengine ya nchini. TSC ilisema uamuzi kuhusu uhamisho wa walimu kutoka kaunti za Mandera na Wajir zitafanywa baadaye.

Hii ni baada ya walimu hao kupiga kambi katika makao makuu ya TSC, Nairobi wakishinikiza wahamishwe kwingineko kwa wakihofia usalama wao.

Visa vya walimu wasio wenyeji kushambuliwa na wahalifu wanaoaminika kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la Al Shabaab vimekithiri zaidi katika kaunti za Kaskazini Mashariki mwa Kenya.

Kisa cha hivi punde kilitokea katika shule ya Kamuthey kaunti ya Garissa ambapo wanamgambo hao waliwaua walimu watatu. Walimu wasio wenyeji ndio wamekuwa walengwa katika mashambulio hayo.

Ingawa, TSC haikutoa idadi kamili ya walimu waliohamishwa, duru zimeiambia safu hii kwamba zaidi walimu 500 wa shule za msingi na za upili walipokea barua za uhamisho.

Kwa mfano, Katibu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Abdirizack Hussein anasema kuwa zaidi ya walimu 30 wamegura Shule ya Upili ya Garissa.

“Takriban thuluthi tatu ya walimu wote wanaofunza katika shule za kaunti ya Garissa hawajazaliwa hapa. Serikali inafaa kutoa usalama kwa walimu kwa sababu kuhamishwa kwa walimu hao kutaathiri pakubwa viwango vya elimu katika kaunti hii,” Bw Hussein akasema.

Afisa huyo wa Knut aliisuta tume hiyo kwa kuwahamisha walimu bila kushauriana na wadau wengine katika sekta ya elimu kama vile vyama vya kutetea masilahi ya walimu na wazazi.

“Sio haki kwa watoto wetu kutarajiwa kufanya mitihani ya KCPE na KCSE ile ile ambayo watoto wa sehemu zingine watafanya mwishoni mwa mwaka huu, ilhali hawatakuwa wameandaliwa ipasavyo kutokana na uhaba wa walimu,” Bw Hussein akaongeza.

Naye Mbunge wa Fafi Bi Sofia Abdinoor anamtaka Waziri wa Elimu George Magoha kuingilia kati suala hilo.

“Tunataka Waziri Magoha afutilie mbali uhamisho huu ambao utawakosesha watoto wetu haki yao ya kikatiba ya kupata elimu. Ni wajibu wa serikali ya kutaifa kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa kote nchini, likiwemo eneo hilo la kaskazini mwa Kenya,” akasema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Elimu Julius Melly anasema usalama ni hitaji muhimu katika utekelezaji wa mipango ya masomo na ipasa kutiliwa mkazo zaidi.

“Inasikitisha kuwa licha ya sekta ya usalama kutengewa fedha nyingi katika bajeti ya kitaifa kila mwaka, serikali kuu imeshindwa kabisa kuhakikisha walimu wanafanya kazi katika mazingira salama. Wiki hii kamati yangu itamwita afisa mkuu mtendaji wa TSC Nancy Macharia na Waziri Magoha kuelezea hali hii,” akasema.