Makala

SEKTA YA ELIMU: Usajili wa walimu kielektroniki utaimarisha usimamizi wao

March 11th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MPANGO wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC) wa kuwasajili walimu kielektroniki kote nchini umetajwa kama ambao utaimarisha utendakazi na usimamizi wa walimu kote nchini.

Kwa mara ya kwanza, viongozi wa vyama vya kutetea masilahi ya walimu na washirika wa maendeleo katika sekta ya elimu wameunga mkono shughuli hiyo miongoni mwa manufaa mengine, itasaidia kubaini idadi kamili ya walimu nchini na sehemu mbalimbali ili kuondoa walimu hewa.

Pia itasaidia kuwafuatilia walimu wenye mienendo ya kutofika kazini. Data ambazo zitakusanywa katika shughuli hii inayoanza leo katika kaunti saba zitaisaidia TSC kuzingatia usawa katika uhamishaji wa walimu na usambazaji wa walimu wapya.

“Usajili huu wa kieletroniki utatusaidia kuhakikisha walimu wamesambazwa kwa usawa ili kuhakikisha kuwa walimu zaidi wanatumwa katika maeneo yenye uhaba mkubwa wa walimu wachache,” anasema mkurugenzi wa TSC anayesimamia Huduma za Usimamizi Ibrahimu Mumin.

Awali, TSC imelaumiwa kwa kutekeleza uhamisho wa walimu bila kuzingatia vigezo muhimu kama hitaji la walimu, umri, afya na masilahi ya kifamilia.

“Usajili wa walimu kieletroniki utaiwezesha TSC kunasa maelezo yote ambayo itaisaidia kufanya maamuzi ya busara wakati wa uhamisho wa walimu. Kwa mfano, itafahamu fika walimu wenye changamoto za kipekee kama vile magonjwa na ambao kuhamishwa kwao kunaweza kuvuruga mfumo wa matibabu,” anasema Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Wilson Sossion.

Naye mkurugenzi mkuu wa shirika la Uwezo Kenya, Emmanuel Manyasa anasema matokeo ya usajili huo mpya unapasa kutumiwa kutatua kero la uhaba wa walimu katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Kenya.

“TSC itafahamu fika idadi ya walimu wa asili ya maeneo hayo na ambao wanafundisha maeneo mengine. Takwimu kama hii itaisaidia kuendesha mpango wa usawazaji wa walimu na uajiri wa wengine wapya ambao wanaweza kufundisha Kaskazini Mashariki bila kutishiwa maisha,” anasema.

Kwa mujibu wa stakabadhi ya TSC kuhusu mpango huu, data za walimu zitakusanywa kutoka ngazi ya mashinani, shule kikiwa kituo cha kwanza cha ukusanyaji.

“Utambuaji wa walimu utaanza katika ngazi ya shule hadi ngazi ya wilaya. Na maelezo yote ya walimu kwenye mitambo ya kieletroniki,” inaeleza hati hiyo.

Hii ina maana kuwa walimu ambao wakati huu huenda wanapokea mishahara bila kuwa na stakabadhi sahihi wataondolewa kwenye orodha ya walimu. Na wale ambao huenda walipata nambari ya usajili ya TSC kwa ulaghai, bila kufuata kanuni iliyowekwa, watatambuliwa na kuondolewa katika orodha ya walimu.

Takwimu ya hivi punde kutoka wa TSC inaonyesha kuwa kuna jumla ya walimu 316,662 katika shule za msingi na za upili kote nchini.

Kati ya hawa, TSC inasema kuwa walimu 217,281 wanafundisha katika shule 22,633 za msingi za umma huku 99,381 wakifunza katika shule 8,865 za upili.

Lakini takwimu hizi zinakinzana na nyingine iliyowasilishwa na TSC mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Elimu wiki jana zilizoonyesha kuwa kuna jumla ya walimu 305,568 katika shule za msingi na upili, za umma, nchini.

Mkinzano katika takwimu hizi mbili unaonyesha huenda kuna walimu hewa nchini, hali inayofanya usajili wa kieletroniki kuwa muhimu.