Makala

SEKTA YA ELIMU: Waliopata alama 350-399 katika hali ngumu wapewe shule za kitaifa

November 20th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BAADA ya matokeo ya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane kutangazwa sasa macho yote yanaelekezwa kwa shughuli ya uteuzi wa wanafunzi watakaojiunga na shule za upili hapo mwakani.

Kulingana na Wizara ya Elimu, shughuli hiyo itaendeshwa chini ya mwongozo ulioanza kutekelezwa mwaka wa 2018 ambapo watahiniwa wote waliopata alama 400 kwenda juu watateuliwa kujiunga na shule 114 za kitaifa humu nchini. Lakini wale waliosomea mazingira magumu na wakapata alama 350 hadi 399 pia huenda wakapata nafasi katika shule hizo.

Kwa hivyo, wanafunzi 9,770 waliopata alama 400 kwenda juu watashindania nafasi katika shule hizo za kitaifa, haswa 20 ambazo zina rekodi ya kuandikisha matokeo mazuri katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne (KCSE).

Baadhi ya shule hizo ni; Alliance Boys, Alliance Girls, Mangu High, Maseno, Starehe Boys, Starehe Girls, Nairobi School, Lenana School na Kenya High School.

Shule zingine zinazovutia wanafunzi wengi ni; Moi Forces Lanet, Moi Forces Academy, Bahati Girls, Moi Girls Eldoret, Nakuru Boys, Loreto Limuru na Limuru Girls. Wazazi wengi wangetaka watoto wao wajiunge na shule hizi na wala sio shule ambazo si maarufu.

Ndiposa akihutubu wakati wa kutangazwa rasmi kwa matokeo ya KCPE katika makao makuu ya Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) Waziri wa Elimu George Magoha alitoa hakikisho kwamba shughuli ya uteuzi wanafunzi utaendeshwa kwa njia haki.

“Ningetaka kutangaza bayana kwamba zoezi la kuwateua wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza litaanza kesho (Jumanne) na kukamilika mnamo Desemba 2. Na shughuli hiyo itaendeshwa kwa njia huru, haki na itakayowaridhisha wanafunzi na wazazi,” akasema Profesa Magoha.

Alitoa hakikisho hili kwa sababu mwaka jana Afisa Mkuu Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Shule za Kibinafsi (KEPSA) Bw Peter Ndoro alilalamika kuwa mfumo wa uteuzi uliwabagua wanafunzi kutoka shule za kibinafsi.

Alidai kwamba watahiniwa wengi, kutoka shule za kibinafsi waliopata alama 400 kwenda juu walikosa nafasi katika shule za upili za kitaifa ilhali wenzao kutoka shule za umma waliopata alama 370 hadi 390 wakiteuliwa kujiunga na shule hizo, hasa “zile za kifahari”.

Hii ni kwa sababu chini ya mfumo uliotumiwa mwaka jana asilimia 70 ya nafasi katika upili za kitaifa zilitengewa wanafunzi kutoka shule za umma huku wenzao wa shule za kibinafsi wakisalia na asilimia 30 pekee. Wizara ya elimu ilitetea mfumo huo ikisema unalenga kuhakikikisha usawa “kwa sababu baadhi ya waliopata alama 370 walisomea katika mazingira magumu na wanafaa kupewa nafasi katika shule za kitaifa.

Mwaka 2019 sawa na mwaka 2018 idadi ya wanafunzi kutoka shule za binafsi waliopata alama 400 kwenda juu ilikuwa juu kuliko wenzao kutoka shule za umma.

Na huenda Bw Ndoro na wenzake wakalalamika tena endapo wanafunzi kutoka shule za umma watatengewa nafasi nyingi katika shule za upili za kitaifa ikilinganishwa na wenzao waliofanya KCPE katika shule za binafsi.

Mshauri wa masuala ya elimu John Mugo anasema hatua ya wizara ya elimu kuamua kwamba watahiniwa wote waliopata alama 400 kwenda juu, wawe kutoka shule za umma au zile za kibinafsi, watajiunga na shule za kitaifa haiwatendei haki wale waliosomea katika mazingira magumu na kupata zaidi ya alama 350 hadi 399.

Dkt Mugo, ambaye ni mkurugenzi wa mipango katika Shirika la Uwezo Kenya anasema wanafunzi waliosomea katika shule za umma walikabiliwa na changamoto kama vile, ukosefu wa madarasa ya kutosha, lishe, walimu na mahitaji mengine ya kimsingi na wakapata alama 350 kwenda wanapasa kuteuliwa katika shule za upili za kitaifa.

“Watoto kama hawa ni werevu na endapo wangesomea katika shule za kibinafsi wana uwezo wa kupata zaidi ya alama 400. Kwa hivyo, wanafaa kupewa nafasi katika shule za kifahari kama Alliance na bila shaka watang’aa zaidi,” anasema.