Makala

SEKTA YA ELIMU: Wazazi wafurahia nafasi ya kubadilisha chaguo la shule

July 10th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MAJUZI, Wizara ya Elimu ilitoa nafasi kwa watahiniwa wa mwaka 2019 wa mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) kufanya mabadiliko ya shule za upili ambazo walikuwa wameteua mapema mwaka 2019.

Waziri Profesa George Magoha alisema aliamuru Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC) kutoa fursa hiyo kwa watahiniwa kwani baadhi yao tayari wamekadiria alama ambazo watapata “katika KCPE kuwa kutokana na alama walizopata katika mitihani ya mwigo”.

Na Katibu wa Wizara ya Elimu Belio Kipsang ametoa hakikisho kuwa kila mwanafunzi ataitwa katika shule mojawapo ya shule ambazo aliteua, kulingana na alama atakazopata katika KCPE mwaka 2019.

Hatua hiyo imeunga mkono Chama cha Kitaifa cha Wazazi (KPA) kinachosema itaondoa shida zilizokumba wazazi mapema mwaka huu baada kugundua kuwa watoto wao waliitwa katika shule ambazo hawakuteua.

“Tunaunga mkono hatua hii ya Wizara kutoa nafasi kwa wanafunzi kubadilisha shule ambazo waliteua ili kuafiki alama zile wanaamini watapata,” anasema mwenyekiti Nicholas Maiyo.

Itakumbukwa kuwa mwaka 2018 wengi wa wanafunzi waliopata alama 400 walivunjika moyo baada ya kukosa kuitwa katika shule za kitaifa ambazo walikuwa wameteua.

Baadhi walikerwa hata zaidi kwa kuteuliwa katika shule za kitaifa za “hadhi ya chini” licha ya waziri wa wizara ya elimu wakati huo kuwapa matumaini ya kuteuliwa katika shule “za ndoto zao”.

Waliovunjika moyo ni wale waliokosa shule za kitaifa zenye sifa kuu, kama vile, Alliance Boys, Alliance Girls, Mangu High, Maseno, Starehe Boys, Starehe Girls, Nairobi School, Lenana School na Kenya High School.

Shule zingine zilizovutia wanafunzi wengi ni; Moi Forces Lanet, Moi Forces Academy, Bahati Girls, Moi Girls Eldoret, Nakuru Boys, Loreto Limuru and Limuru Girls.

Mwalimu mkuu wa shule moja ya upili katika kaunti ya Nairobi anasema hali hii ya wanafunzi waliopita kwa alama za juu kukosa nafasi katika shule walizochagua husababishwa na ufisadi katika mchakato wa uteuzi.

Vilevile, anaongeza, shughuli hiyo huingiliwa na watu mashuhuri serikali ambao huwashinikiza walimu wakuu kuwatengea nafasi katika kidato cha kwanza.

“Ni siri iliyo wazi kwamba baadhi ya maafisa wakuu serikali wakiwemo mawaziri huwalazimisha walimu wakuu wa shule za kitaifa zenye hadhi ya kuu kuwatengea nafasi kadha. Kando na hayo baadhi yao kupokea mlungula kutoka kwa wazazi matajiri,” anasema mwalimu huyo ambaye aliomba tusichapishe jina lake.

Hii ndio hali iliyopelekea, kwa mfano, watahiniwa 15 wa shule ya Bethany Chrsistian Academy waliopata alama 400 na zaidi kukosa nafasi katika shule za kitaifa ambazo walichagua. Shule hiyo ilikuwa ya pili bora kitaifa kwa kuandikisha alama ya wastani ya 417 nyuma ya Fred’s Academy kutoka Meru iliyopata alama ya 419.

Mwanafunzi asikitika

Kwa mfano, Ruth Chaka, 14, aliyepata alama 446 na kuorodheshwa mwanafunzi wa tatu bora kitaifa na bora zaidi katika eneo la Pwani alikosa kujiunga na shule ya upili chagua lake la kwanza, Alliance Girls.

Badala yake msichana huyo aliteuliwa na shule ya Upili ya Mama Ngina Girls ambayo haikuwa miongoni mwa shule ambazo alichagua.

“Nahisi vibaya kwa kunyimwa nafasi katika shule ya Alliance Girls ambayo nimekuwa nikitamani,” Chaka alinukuliwa akisema akiitaka Wizara iingilie kati suala hilo ili aweze kupewa nafasi katika shule hiyo ambayo huandikisha matokeo mazuri katika mitihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE).

Mtaalamu wa masuala ya elimu John Mugo anasema hali hii huchangiwa na ushindani mkubwa wa nafasi katika shule 18 za kitaifa za zamani kando na zimwi la ufisadi ambalo huingilia shughuli zima ya uteuzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza.