Makala

SEKTA YA ELIMU: Yakini, ufichuzi kwamba baadhi ya kozi vyuoni hazifai wavunja moyo

February 20th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MATOKEO ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) yanapotangazwa kila mwaka, hamu kubwa ya wazazi wa watahiniwa huwa ni kuona kwamba watoto wao wamepata alama za kuwawezesha kujiunga na vyuo vikuu kusomea kozi ambazo zitawawezesha kupata ajira siku za usoni.

Hata hivyo, ufichuzi kwamba baadhi ya kozi zinazofunzwa katika vyuo vikuu vya umma ‘hazina maana’ kwani hazijaidhinishwa na Tume ya Kusimamia Elimu ya Vyuo Vikuu (CUE) unawavunja moyo wazazi na wanafunzi.

Tume hiyo inasema kuwa jumla ya kozi 133 zinazofunzwa katika vyuo vikuu vya umma na kibinafsi humu nchini ni batili kwani haijaziidhinisha inavyohitajika kisheria.

Hii ina maana kuwa zaidi ya wanafunzi 10,000 ambao tayari wanasomea kozi hizo huenda wakalazimishwa kukatiza masomo yao kwa sababu ya kubainika makosa ambayo sio yao.

Isitoshe, inaashiria kuwa wanafunzi hao wamepoteza pesa na muda wao wakisomea kozi za shahada ambazo hazitambuliwa katika soko la ajiraKimsingi, ni wajibu wa CUE kuidhinisha kozi zote zinazofunzwa katika vyuo vikuu.

Katika kutekeleza kazi hii, wakaguzi wa tume hii huhakikisha kuwa kuna kabla ya chuo kikuu kuanza kufunza kozi fulani huwa kimejiandaa sawasawa kwa kununua vifaa na kuajiri wakufunzi wa kutosha.

Sasa swali ni je, mbona tume hii ilisubiri vyuo husika kuanza kufunzisha kozi fulani na kisajili wanafunzi kisha inatuma wakaguzi wake kuziharamisha?

Pili, mbona CUE ikatoa habari hiyo kwa vyombo vya habari bila kutaja kozi husika ambazo ilibaini kuwa batili?

Hali hii bila shaka itasababisha taharuki na wasiwasi kubwa miongoni mwa wanafunzi katika vyuo vikuu.

Wazazi wao wanafunzi hao pia wataingiwa na tumbojoto wakitaka kujua ikiwa kozi ambazo watoto wao wanasomea ni halali au la.

Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Kisii, ambako jumla ya kozi tano zimebainika kuwa haramu, anailamu CUE kwa kuchochea makabiliano kati ya wanafunzi na vyuo husika.

“Ni makosa kwa tume hii kudai kuwa kufuatia ukaguzi ambao ilifanya katika vyuo vikuu nchini mwaka 2018, iligundua kuwa kozi 133 sio halali. Hii ina maana kuwa imekuwa ikizembea kazini. Mbona ikasubiri vyuo kuanza kufunza masomo hayo ndipo ianze kufanya ukaguzi wake? Wanafunzi sasa watawalaumu wasimamizi wa vyuo ilhali kosa ni la CUE,” akasema mhadhiri huyo ambaye aliomba tulibane jina lake.

Uchunguzi umebaini kuwa uchu wa kuchuma fedha ndio imepelekea baadhi kuanzisha kozi kiholela bila kuzingatia kanuni iliyowekwa.

Kisingizio hapa huwa ni ufinyu wa ufadhili kutoka kwa serikali haswa kwa vyuo vikuu vya umma. Hii ni kwa sababu tangu mwaka wa 2000 serikali imekuwa ikianzisha vyuo vikuu bila mpangilio madhubuti, aghalabu kutokana na msukumo wa kisiasa.

?Kwa hivyo, wa kulaumiwa katika hali hii ambapo rasilimali zinapotezwa kwa kozi zisizo na maana ni serikali, CUE na hata vyuo vyenyewe.