Habari Mseto

Sekta ya SMEs yatengewa mgao kuinusuru mawimbi ya Covid-19

June 12th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

SEKTA ya biashara ndogondogo na zile za kadri – SMEs – imetengewa Sh10 bilioni zitakazotumika kama mikopo kuziimarisha.

Alhamisi, akisoma makadirio ya bajeti mwaka wa fedha 2020/2021, Waziri wa Fedha na Hazina ya Kitaifa Ukur Yatani alisema fedha hizo zitaelekezwa kwa wafanyabiashara wa sekta hiyo ya Juakali kama mikopo ili kuipa afueni kufuatia athari za Covid – 19, zinazoendelea kuiyumbisha.

Mbali na Sh23.1 bilioni zilizokuwa zimepitishwa na bunge la kitaifa awali kupiga jeki sekta hiyo, Waziri pia alitangaza mgao mwingine wa Sh10 bilioni kwa sekta hiyo, akifafanua kwamba fedha hizo zitasaidia kuipunguzia mzigo mzito wa ushuru (VAT).

Migao hiyo kwa sekta ya SMEs, ilitajwa katika mojawapo ya vigezo nane chini ya makadirio ya bajeti 2020/2021 yenye mada “Kukuza Uchumi”, kufuatia athari za janga la Covid – 19 kwa uchumi na sekta mbalimbali, biashara ikiwemo.

Licha ya sekta ya Juakali kupata mgao huo, wafanyabiashara wanasema fedha hizo huwa haziwafikii, kwa mujibu wa makadirio ya bajeti miaka ya awali. “Huu si mwaka wa kwanza tumeskia wafanyabiashara wa kiwango cha chini wakitengewa mgao kutumika kama mikopo kutuimarisha, umewahi kutufikia. Ili kusaidia kila mfanyabiashara, kodi (akimaanisha ushuru) wa bidhaa za juakali ingepunguzwa zaidi,” Zipporah Ndereba, muuzaji wa nguo Nairobi, akaambia Taifa Leo katika mahojiano.

Kustawisha sekta ya juakali, waziri Yatani pia alisema serikali inalenga kupiga jeki soko la bidhaa zinazotengenezewa humu nchini.

“Mpango huu unapania ‘kununua Kenya na kujenga Kenya’, kwa kuimarisha soko la bidhaa zinazoundiwa humu nchini,” Bw Yattani akaeleza, akisoma makadirio hayo ya bajeti katika bunge la kitaifa.

Akikiri sekta ya Juakali, na ambayo imewakilisha asilimia 75 ya nguvu kazi nchini, imeathirika kwa kiasi kikuu kufuatia mkurupuko wa virusi vya corona, Waziri alisema serikali imeweka mikakati maalum kuiimarisha.

Mbali na uchumi kuathirika, janga la Covid-19 limesababisha watu kupoteza nafasi za kazi na pia biashara na mikahawa kufungwa.

Waziri Yattani alisoma makadirio ya bajeti ya Sh2.790 trilioni, mwaka wa Fedha 2020/2021.