Habari Mseto

Sekta ya utalii katika hatari walaghai wakiibia wageni

August 10th, 2019 2 min read

Na EDWIN OKOTH na KALUME KAZUNGU

MATAPELI wanaosingizia kuwa mawakala wamewalaghai mamia ya watalii kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni na kuhatarisha sura ya Kenya kama kivutio cha watalii.

Walaghai hao hutumia kampeni feki mitandaoni zinazoambatana na wasifu na mipango ya bajeti ya kuvutia kuwahadaa raia wa kigeni wanaotuma sehemu ya malipo kwanza kabla ya kuachwa Kenya mara wanapolipa hela zilizosalia.

Taifa Jumapili pia imefahamu kwamba shirika hilo la mabwenyenye lililokita mizizi limetia makali ujuzi wa kuwakwepa maafisa wa polisi kwa kubadilisha majina, magari ya wafanyakazi na watalii, kabla ya kujitokeza wakati wa msimu wa juu ili kufyonza mamilioni kutoka kwa watalii wasio na habari wanaozuru taifa.

Mhasiriwa mmoja wa hivi majuzi katika sakata hiyo ni Bw Chen Dong Yuan, mhandisi wa asili ya Uchina mwenye umri wa miaka 51 kutoka Changsha, aliyejawa na furaha kutembea Kenya kwa kutumia safari za ndege za moja kwa moja zilizozinduliwa na shirika la ndege la China Southern Airlines mnamo Juni, 2019.

Bw Chen hakujua kilichomsubiri pamoja na marafiki wake watano baada ya kupanga na kulipa asilimia 50 kwa kampuni ya Kenya Walking Survivors Safaris Limited kwa siku nane katika vivutio vya utalii kote nchini. Hiyo ilikuwa ni mwanzoni mwa Julai.

“Tulienda afisini mwao ambapo nililipa karibu Sh295,000 ambazo alisisitiza zilipaswa kuwa pesa taslimu. Kisha tulielekea Amboseli kwa siku mbili kulingana na ratiba. Gari na dereva alibadilishwa baada tu ya kutoka Nairobi na tulipokuwa tukirejea dereva akatueleza kampuni iliyotukabidhi kwake ilikuwa imefunga shughuli zake ghafla na ziara yetu haingeendelea isipokuwa tufanye mipango mipya,” alisema Chen.

Kwingineko, bodi ya Udhibiti wa Vyombo vya Baharini (KMA) imewatahadharisha mabaharia dhidi ya kutumia eneo ambako uchimbaji wa viegesho vya Bandari Mpya ya Lamu (LAPSSET) unaendelea eneo la Kililana na Manda Bay, Kaunti ya Lamu.

Katika ujumbe kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu wa KMA, George Okong’o, aliwataka mabaharia wanaotumia Bahari Hindi eneo la Lamu kuwa waangalifu na kuepuka kutekeleza shughuli zao karibu na eneo la ujenzi wa LAPSSET ambako kuna vifaa vizito ndani ya bahari vinavyotumika kuchimbia viegesho vya LAPSSET.

Bw Okong’o alisisitiza kuwa kuendelea kuendesha boti karibu na Kililana na Manda Bay kutawatumbukiza mabaharia pabaya kwani huenda wakaishia kugongana na vifaa hivyo baharini na kusababisha ajali mbaya na hata maafa.

“KMA inawatahadharisha mabaharia wote wanaotumia Bahari Hindi eneo la Lamu kwamba kuna maboya ambayo yamefungiwa vifaa vizito vinavyotumika kwa uchimbaji wa viegesho vya LAPSSET hasa eneo la Kililana na Manda Bay. Tunawasihi waendeshaji boti na mashua kuwa waangalifu. Waepuke kuendesha vifaa vyao karibu na maeneo hayo ili wasigongane na maboya na vifaa vizito na kusababisha ajali na maafa,” akasema Bw Okong’o.

Tangazo la KMA linajiri wakati ambapo wahudumu wa boti na mashua, Kaunti ya Lamu wamekuwa wakiishiniukiza serikali kupitia bodi ya ujenzi na uendelezi wa LAPSSET, kuwafidia hasara kwani ujenzi wa LAPSSET huenda ukachangia kufungwa kwa baadhi ya njia za baharini ambazo waendeshaji bpti na mashua eneo hilo la Lamu wanatumia.

Kaunti ya Lamu iko na zaidi ya waendeshaji boti na mashua 5000 wanaoishi kwenye visiwa mbalimbali vya eneo hilo.