Habari Mseto

Sekta ya uvuvi kuimarishwa nchini

August 26th, 2020 1 min read

Na WINNIE ATIENO

WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Peter Munya amesema vijana 2,000 watapewa mafunzo ya ubaharia ili waweze kufanya kazi kwenye mashua za uvuvi.

Waziri Munya alisema kuna haja ya sekta hiyo kuwa na wataalam wa uvuvi ambao watafanya kazi baharini kwenye mashua za uvuvi kuimarisha sekta hiyo.

Alisema sekta ya uvuvi wa baharini ina uwezo wa kuajiri mamia ya vijana.

Hata hivyo alilalamika akisema idadi kubwa ya vijana hao hawana tajriba ya uvuvi ili kuchukua nafasi zilizoko.

Bw Munya alisema serikali imeweka mikakati kuimarisha sekta ya uvuvi ili kuleta maendeleo nchini.

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Peter Munya akiwa Liwatoni. Picha/ Winnie Atieno

Akiongea alipozuru kituo cha Liwatoni ambacho ni maalum kwa kuimarisha sekta ya uvuvi na kilichogharimu serikali Sh318 milioni kukirekebisha, Bw Munya alisema wizara yake imeanza kuwalinda wavuvi na kuimarisha sekta hiyo ili kufufua uchumi wa taifa.

Bw Munya ambaye aliandamana na maafisa wakuu serikali kuzuru sehemu hiyo huko Mombasa Bw Munya alisema asilimia 30 ya samaki itakayovuliwa baharini itauzwa kwa bei ya reja reja huku 70 ikisafirishwa kuuzwa nchi za kigeni.

“Liwatoni itabadilisha na kuimarisha sekta ya uvuvi nchini na hivi karibuni kituo hiki kitaanza kazi ambapo mashua za uvuvi zitatia nanga eneo hili kuleta samaki. Itakuwa na uwezo wa kuweka tani 250 za samaki lakini tunapania kupanua ili kufikia tani 500,” alisema Bw Munya.