Michezo

Semedo ajiengua Barcelona na kutua Wolves kwa Sh5.2 bilioni

September 23rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

WOLVERHAMPTON Wanderers wamemsajili beki wa kulia raia wa Ureno, Nelson Semedo kutoka Barcelona kwa kima cha Sh5.2 bilioni.

Kocha Nuno Espirito Santo wa Wolves amekuwa akimsaka beki wa kujaza nafasi ya Matt Donerty aliyeyoyomea kambini mwa Tottenham Hotspur mwezi uliopita.

“Si rahisi kupata fursa ya kumsajili mwanasoka wa haiba kubwa wa kiwango cha Semedo,” akasema Mwenyekiti wa Wolves, Jeff Shi.

Semedo, 26, amechezea Barcelona mara 124 na kuwajibishwa mara 13 na timu ya taifa ya Ureno.

Semedo amerasimisha uhamisho wake hadi Wolves kwa mkataba wa miaka mitatu na anakuwa mchezaji wa tatu kuingia katika sajili rasmi ya kikosi hicho baada ya Fabio Silva na Ki-Jana Hoever waliotokea FC Porto na Liverpool mtawalia.

Uhamisho wa Semedo unafanya kuwa mwanasoka ghali zaidi kuwahi kusajiliwa na Wolves baada ya kikosi hicho kutoa Sh4.9 bilioni kwa minajili ya huduma za Silva.

“Wolves walisajili matokeo ya kuridhisha msimu uliopita wa 2019-20 na miongoni mwa vikosi vinavyoinukia vyema zaidi katika soka ya Uingereza na bara Ulaya. Naamini kwamba nitawasaidia Wolves kupanda zaidi kwenye jedwali la EPL baada ya kuambulia nafasi ya saba msimu jana,” akasema Semedo.

“Nuno ni kocha mzuri ambaye amefanya mambo makubwa hapa Wolves na katika vikosi vyote vingine ambavyo amewahi kuvinoa. Nina uhakika wa kujifunza mengi zaidi kutoka kwake nikiwa uwanjani Molineux sasa,” akaongeza.