HabariSiasa

Seneta aunga mkono wito Wakenya wafungiwe nyumbani

April 4th, 2020 2 min read

BENSON AMADALA na VITALIS KIMUTAI 

SENETA wa Kakamega, Cleophas Malala, ameunga mkono kauli ya Chama cha Walimu Nchini (KNUT) kwamba, Rais Uhuru Kenyatta anafaa atangaze amri ya kutoka nje usiku na mchana ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Bw Malala ameonya kwamba, hilo lisipofanyika, basi Wakenya wataathirika zaidi na virusi hivyo ambavyo tayari vimesababisha vifo vya watu wanne nchini.

Japo Knut ilipendekeza kafyu kamili ya kutoka nje itangazwe kisha idumu kwa siku 21, Bw Malala alipendekeza marufuku hiyo iwekwe kwa siku 14 pekee jiini Nairobi ambapo visa vingi vya corona vimeripotiwa.

Aidha, seneta huyo wa chama cha ANC alipendekeza serikali izime magari ya uchukuzi ya umma dhidi ya kuwasafirisha abiria kutoka jijini Nairobi hadi mashinani kwa kipindi hicho kama njia ya kuzuia kuenea kwa maambukizi hayo.

“Natoa wito kwa serikali ili kuhakikisha inatekeleza mikakati ambayo itazuia kusambaza zaidi kwa virusi vya corona. Mojawapo ya njia hizo ni kufunga kabisa jiji la Nairobi na kuweka kafyu ya kutotoka nje kwa siku 14. Hii ni kwa sababu Nairobi ndiyo imegeuka kitovu cha maambukizi ya virusi hivyo hatari na vitasambaa hadi maeneo mengine tahadhari isipochukuliwa,” akasema Bw Malala.

“Hata hivyo kafyu hiyo haifai kuwahusisha watu wanaotoa huduma spesheli na malori yanayosafirisha bidhaa au vyakula kutoka bandari ya Mombasa hadi Nairobi. Serikali kuu ndiyo itaamua watu wa kutoa huduma hizo muhimu ili wanaougua wasitatizike,” akaongeza.

Bw Malala ambaye tayari ametangaza azma yake ya kuwania ugavana wa jimbo la Kakamega, pia alirai serikali kusambaza barakoa na sanitaiza mashinani na mijini ili kuhakikisha wenye virusi hivyo hawavisambazi kwa wengine kwa urahisi.

“Kama kiongozi aliyechaguliwa na anayewakilisha kaunti ambayo iko mashinani, ninaomba serikali itangaze marufuku ya kutoruhusu magari kutoka jijini hadi maeneo mengine ya nchi ambayo yamesajili idadi ndogo ya walioathirika na virusi hivi hatari,” akasema.

Knut ilikuwa imeirai serikali ihakikishe kafyu ya usiku na mchana inawekwa kwa siku 21 kisha Wakenya warejelee maisha yao ya kawaida baada ya hapo.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Sossion alimtaka Rais Uhuru Kenyatta awe na ujasiri wa kutosha na kuweka kafyu ya usiku na mchana ili kuokoa taifa hili ambapo uchumi wake utazidi kudorora janga la virusi vya corona likiendelea.

“Kafyu kamili ni chungu na huenda ikawataabisha wengi lakini kwa sasa huo ndio mwelekeo unaofaa kuchukuliwa kuzuia maambukizi zaidi ya virusi hivi ambavyo sasa vimesambaa nchini.

Hilo lisipofanyika, maambukizi mapya yatatokea na watakaoathirika watakuwa wengi,” akasema Bw Sossion mjini Bomet.

Mbunge huyo maalum aliongeza kwamba, ilikuwa bayana Wakenya wengi katika maeneo mbalimbali hawajamakinikia usafi na mikakati mingine iliyowekwa na wizara ya afya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya corona ndiyo maana kafyu hiyo inafaa ikumbatiwe.

Vilevile alisema kafyu kamili itazuia shule na taasisi za masomo kugeuzwa vituo vya kuwapa hifadhi watu waliopatikana na virusi vya corona.? “Lazima kama Wakenya tukubali kuteseka kwa muda mfupi na kuokoa maisha yetu. Hii ndiyo njia itakayosambaratisha kuenea kwa virusi hivi nchini,” akaongeza.