Makala

Seneta Joe Nyutu kufadhili ubunaji wa sheria ya mikopo bila riba kwa walemavu

April 21st, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

SENETA wa Murang’a Joe Nyutu amesema atafadhili ubunaji wa sheria ya kuweka ulazima wa taasisi za kifedha kutoa mikopo bila riba kwa watu wanaoishi na ulemavu.

Amesema kwamba ikiwa serikali huwa haiwatozi walemavu ushuru wa uagizaji bidhaa na pia leseni za kibiashara, hata benki zinafaa kushinikizwa ziifanye sheria kwamba mikopo kwao haitakuwa na riba yoyote.

Aidha, amependekeza kwamba kampuni zote zinazohudumu hapa nchini ziwe zikitenga asilimia 20 ya bajeti za manufaa kwa jamii (CSR) kwa walemavu.

“Inafaa iwe sheria kwamba kampuni hizi ziwe zikielekeza mipango yao ya miradi kwa jamii kwa walemavu kwa kiwango kisichopungua asilimia 20 ya bajeti zao za kila mwaka,” akasema.

Bw Nyutu alikuwa akiongea katika mkutano wa wadau wa kupanga mikakati ya kutoa vijigari ambavyo vimeundwa kama vioski kwa walemavu wa Murang’a.

Mnamo Ijumaa, Bw Nyutu alitoa vijigari 200 kwa walemavu katika wadi mbalimbali za kaunti hiyo katika hafla iliyofanyika katika mji wa Maragua na Wakfu wa Joe Nyutu.

Bw Nyutu alitoa vijigari hivyo vikiwa pia na bidhaa za uchuuzi ambapo mlemavu anaweza akageuza kijigari chake kuwa duka.

Bw Nyutu alisema kwamba walemavu wanaweza wakafuga nguruwe, samaki, kuku na sungura kwa kuwa sekta hizo hazihitaji nguvu nyingi za kimwili.

Pia, alisema wanaweza wakashiriki biashara za uchuuzi ndani ya maduka au hata katika sekta ya jua Kali bora tu wapewe mtaji.

Aidha, amezitaka hospitali zote nchini zishuritishwe kuzindua karakana za kufanyia ufundi pasipo malipo yoyote vifaa ambavyo walemavu hutumia.

Alisema kwamba walemavu huhangaika sana wakati vifaa vyao vya kuwasaidia kutembea, kuketi na kusimama vimeharibika kwa kuwa hakuna mafundi spesheli wa kuvikarabati.

“Hii ina maana kwamba serikali za Kaunti zihakikishe zimeajirj mafundi wa vifaa vya walemavu kama mikongojo, vijigari, viatu spesheli na pia mikwanju ya vipofu,” akasema.

Alisema ufundi huo unafaa kuwa katika hospitali kwa kuwa utaalamu wa madaktari huhitajika katika ulainishaji wa vifaa hivyo.

“Na kwa kuwa hatuwezi tukawatuma madaktari wakahudumu katika karakana nje ya hospitali, tunafaa kuwa na sera ya kutenga nafasi katika uwanja wa kila hospitali ya umma kushirikisha utaalamu huo,” akasema.

Mshirikishi wa PLWDs katika eneobunge la Maragua Bi Damaris Irungu alisema kwamba kuna haja ya walemavu hata kupewa kazi za kaunti.

“Tuko na walemavu ambao wamesoma na walio na uwezo kamili wa kuchapa kazi za ofisi. Lakini huwa tunatengwa kama wanaofaa tu kusaidiwa kwa kutekelezewa maombi na kuonyeshwa huruma,” akasema.

Bi Irungu aliwataka viongozi kuweka mikakati ya kuwajumlisha walemavu katika maamuzi muhimu ya kiutawala huku akishabikia mapendekezo ya Bw Nyutu.