HabariSiasa

Seneta Khaniri amtaka Raila ampishe aongoze NASA

March 4th, 2018 1 min read

Na PIUS MAUNDU

SENETA wa Vihiga, Bw George Khaniri, ameanza kampeni ya kumrithi kinara wa NASA Raila Odinga.

“Ikiwa hamuwezi kuwafikisha Wakenya Kanaani, anzeni kujiandaa kunikabidhi uongozi mimi na seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior,” alisema Bw Khaniri akiwarejelea mabwana Raila Odinga na Kalonzo Musyoka

Kulingana na seneta huyo, wakati umefika kwa NASA kuongozwa na viongozi wengine ili iweze kutimiza malengo yake.

Akizungumza alipohudhuria mazishi katika kijiji cha Kiatinineni, Kaunti ya Makueni mwishoni mwa wiki, Bw Khaniri alimsifu Seneta Kilonzo na kumtaja kama shujaa wa siasa za Ukambani.

Matamshi yake yalijiri huku muungano wa NASA ukikumbwa na mgawanyiko kufuatia hatua ya vinara wenza kususia hafla ya kiapo cha Bw Odinga kuwa ‘rais wa wananchi’ iliyofanyika Uhuru Park mnamo Januari 30.

Huku Bw Odinga na chama chake cha ODM kikidai haki katika uchaguzi wa mwaka 2017, vinara wenza Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula wanataka mjadala kuhusu siasa za uchaguzi wa 2022.

Bw Khaniri alisema NASA itatatua mzozo uliopo na kwamba muungano huo unaweza kudumu hata bila Bw Odinga na Bw Musyoka.

Maseneta hao walishtumu serikali ya Jubilee wakisema utawala wake umevuruga uchumi wa nchi. Walisema NASA inafaa kulenga vita dhidi ya utawala mbaya.

Hata hivyo walitofautiana kuhusu mageuzi ya katiba kulingana na mswada ambao mbunge wa Tiaty William Kamket anapendekeza, ambapo Bw Khaniri alikubaliana nao, naye Bw Kilonzo akaupinga.

“Wakati umefika tuunde nafasi zaidi za uongozi ili kupunguza mamlaka ya rais,” alisema Bw Khaniri.

Bw Kilonzo Jnr alisema kinachohitajika ni mageuzi ya kikatiba ya kuimarisha ugatuzi kwa kutengea serikali za kaunti pesa zaidi na kuwa na mahakama huru.