Habari Mseto

Seneta Ledama ole Kina aitwa mahakamani ajibu shtaka la uchochezi

May 19th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

SENETA wa Kaunti ya Narok Ledama ole Kina ameagizwa afike kortini Juni 2, 2020, kujibu mashtaka ya kuchochea uhasama miongoni mwa makabila mbalimbali yanayoishi katika kaunti hiyo.

Agizo afike katika mahakama ya Milimani limetolewa Jumanne na hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot.

Akiwasilisha ombi la Bw Ole Kina aagizwe afike mahakamani kiongozi wa mashtaka Bw James Gachoka, amesema mwanasiasa huyo hakuwa amekabidhiwa samanzi afike kortini.

“Kama ilivyo desturi na mashiko ya kisheria kabla ya mmoja kushtakiwa anaarifiwa ndipo ajiandae kimawazo na pia awasiliane na mawakili wake. Idara ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ilikuwa haijamkabidhi mshukiwa huyu samanzi afike kortini kujibu shtaka,” akasema Bw Gachoka.

Bw Gachoka ameomba afisi ya DPP ipewe muda wa wiki mbili kumsaka Bw ole Kina na kumkabidhi samanzi afike kortini Juni 2, 2020.

Mahakama imefahamishwa tayari shtaka dhidi ya Seneta huyo limetayarishwa.

“Shtaka atakalojibu mshukiwa huyu limetayarishwa na hata limeidhinishwa na afisi ya DPP,” Bw Cheruiyot amefahamishwa.

Shtaka dhidi ya ole Kina linadai mnamo Februari 19, 2020, katika kituo kimoja cha televisheni alitoa matamshi yaliyolenga kuibua hisia za uhasama baina ya jamii ya Wamaasai na makabila yanayoishi katika Kaunti ya Narok.

Shtaka linadai mwanasiasa huyo alidai kuwa maslahi na masuala ya jamii ya Wamaasai yatatuliwa na wao wenyewe na wala sio akina ‘Manje’ wanaojidai wanaweza kusikizwa na viongozi kutoka eneo la Mlima Kenya.

Hisia za uchochezi

Shtaka hilo lilisema kuwa matamshi hayo yalilenga kuzua hisia za uchochezi wa jamii ya Wamaasai na makabila mengine yanayoishi katika Kaunti ya Narok.

Mahakama imefahamishwa uchunguzi ulifanywa na kukamilishwa na Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Mshikamano wa Kijamii (NCIC) miezi miwili iliyopita.

Mahakama imekabidhiwa nakala za shtaka hilo na kuombwa imwamuru ole Kina afike kortini Juni 2, 2020.

Akitoa agizo Bw Cheruiyot amesema amesoma shtaka dhidi ya mwanasiasa huyo na kuridhika lina mashiko kisheria ayajibu.

Mahakama imemwagiza DPP amkabidhi mshukiwa huyo samanzi afike kortini.

Ole Kina alianza kusakwa baada ya matamshi yake wakati watu walifukuzwa katika msitu wa Mau, Kaunti ya Narok mapema mwaka 2020.

Maelfu ya wakazi waliokuwa wamenyakua vipande vya ardhi katika msitu huo wa Mau walitimuliwa na shule za humo kufungwa katika jitihada za kuhifadhi chemchemi hiyo ya maji.