Siasa

Seneta Ledama Ole Kina aruhusiwa kuvaa mavazi ya kimaasai bungeni

November 10th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Seneti Kenneth Lusaka ametoa uamuzi kwamba maseneta wanaruhusiwa kuvalia mavazi ya kitamaduni Bungeni.

Hii ni baada ya Jumanne alasiri Seneta wa Narok Ledama Ole Kina kuibua msisimko na shutuma kutoka kwa wenzake alipoingia katika ukumbi wa mijadala, akiwa amevalia mavazi ya kitamaduni ya jamii ya Maasai.

Malalamishi kutoka kwa maseneta waliotaka Bw Ole Kina afurushwe kwa kutovalia mavazi yanayotambuliwa na kanuni za bunge hilo, ndiyo yalimfanya Bw Lusaka kutoa taarifa kuhusu iwapo Seneta huyo wa Narok alikuwa amevalia vizuri au la.

“Bw Spika, Seneta Ledama amevalia mavazi ya Kimaasai ilhali kulingana na kanuni za bunge  wanaume wanapaswa kuvalia suti na tai. Je, hiyo ni sawa kwa sababu kila moja wetu anaweza kuingia hapa tukiwa tumevalia kila aina ya mavazi yanayolandana na tamaduni ya jamii zetu?” akauliza Seneta wa Wajir Abdullahi Ali.

Japo kanuni za Seneti zinatambua suti na tai kama mavazi rasmi kwa maseneta wanaume, nyakati zingine maseneta Waislamu huingia ukumbini na kushiriki mijadala wakiwa wamevalia mavazi ya kidini maarufu kama “kanzu”.

Lakini akimjibu Seneta Ali na mwenzake waliokanganyikiwa kuhusu uhalali wa vazi la Bw Ole Kina, Spika Lusaka alisema mavazi ya kimatamaduni yanaruhusiwa kwani “Seneti inawakilisha kila kaunti yenye mavazi yake ya kitamaduni.”

Bw Lusaka alisema Katiba ya Kenya na taratibu za Afisi ya Spika zinatambua utamaduni.

“Sote tunajua kuwa tunawakilisha kaunti zetu; na kila kaunti ina mavazi yake ya kitamaduni. Kaunti za Narok na Kajiado zina mavazi yao ya kitamaduni ambayo yanatambuliwa kote ulimwenguni. Kwa hivyo, haitakuwa jambo la busara kwangu kumwamuru Seneta Ledama Ole Kina aondoke kwa misingi ya kuvalia visivyo,” akaeleza.