Makala

Seneta mcheshi anayetumia kicheko kama ‘dawa’ ingawa ashawahi kujipata motoni

April 2nd, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

YEYE ni mwanasiasa, lakini anakiri kwamba, asingalikuwa mwanasiasa, pengine angekuwa mcheshi.

Hiyo ndiyo sifa ya Seneta John Methu wa Kaunti ya Nyandarua.

Ingawa kazi ya Useneta inahitaji mtu mkakamavu, Bw Methu anasema majukumu yake ya kikazi huwa hayamzuii kuwa mchangamfu, hasa wakati anapoingiliana na watu.

“Ni kweli kuwa nyakati nyingine tunafaa kutocheka na mtu, hasa tunapojadili masuala muhimu yanayohusu nchi na maslahi ya watu wetu. Hata hivyo, mwishowe huwa tunatangamana na wananchi. Huwa tunatangamana nao katika hafla tofauti kama harusi au mikutano ya hadhara. Wao hutueleza mambo yanayoendelea katika maeneo ya mashinani. Wao ndio mabosi wetu. Mbona mtu asiwe mchangamfu na hata kuwachekesha ikiwezekana?” akasaili Bw Methu kwenye mahojiano na Taifa Dijitali mnamo Jumatatu Aprili 1, 2024.

Si mara moja ambapo seneta huyu amezua vicheko mbele ya viongozi kama Rais Willam Ruto na Nabu Rais Rigathi Gachagua.

Mnamo Oktoba 18, 2023, Seneta Methu alizua kicheko miongoni mwa watu waliokuwa wamehudhuria hafla moja ya Kanisa la Kianglikana  Kenya (ACK), eneo la Ol Kalou, aliporejelea ‘ugumu’ aliopitia katika kumwoa mkewe, ambaye ni wa dhehebu la ‘Akorino’.

“Nimefanya majukumu mengi magumu katika maisha yangu. Hata hivyo, kumrai mke wangu kukubali nimwoe kilikuwa kibarua kigumu sana. Unajua wanawake wa dhehebu hilo huwa wagumu sana kuamini kwamba mwanamume asiyejifunga kilemba kichwani hawezi kuwa mwajibikaji,” akasema Bw Methu, kwenye hafla hiyo iliyohudhuriwa na Bw Gachagua.

Mamia ya watu waliokuwa wamehudhuria hafla hiyo walianguka kwa vicheko.

Ni kwenye hafla hiyo ambapo mwanasiasa huyo alimtambulisha mkewe hadharani kwa mara ya kwanza.

Mnamo Oktoba 29, 2023, Seneta Methu alizua kicheko miongoni mwa watu waliokuwa wamehudhuria hafla ya maadhimisho ya miaka 40 ya uwepo wa kanisa la ACK katika Kaunti ya Uasin Gishu.

Akihutubu, Bw Methu alimshukuru Rais Ruto kwa mpango wake wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu kuwafaidi Wakenya, akisema hata Biblia inasema Yesu alienda kujengea Wakristo makao mengi mbinguni.

Kauli hiyo ilizua kicheko kwa karibu kila mtu, akiwemo Rais Ruto.

Kicheko chake, hata hivyo, kimewahi mtia matatani akikaangwa mitandaoni kufuatia kauli ya ‘kikabila’ aliyotoa.

Kutokana na sifa yake ya ucheshi, baadhi ya maseneta wake wanasema wamempa msimbo wa ‘Seneta Mcheshi’.

Seneta Karungo Thang’wa wa Kaunti ya Kiambu, anamtaja Bw Methu kuwa kiongozi wa kipekee ambaye “huwachangamsha kila mara baada ya vikao vya Seneti au kamati tofauti za Seneti.”

“Huwa tunakimbia kwake atupe simulizi za kuchangamsha. Ni kiongozi wa kipekee,” akasema Bw Thang’wa.

Bw Methu, ambaye ni miongoni mwa maseneta wachanga zaidi nchini, anasema kuwa mazingira magumu aliyolelewa ndiyo yamemfanya kukumbatia ucheshi kama njia ya kuyafanya maisha kuwa ya furaha.