Habari Mseto

Seneta Murkomen mwingi wa bashasha baada ya kufanyiwa upasuaji salama

September 20th, 2019 1 min read

Na MARY WANGARI

SENETA wa Elgeyo-Marakwet, Kipchumba Murkomen amejawa na bashasha baada ya kufanyiwa upasuaji salama kufuatia jeraha alilopata majuzi katika mechi ya kirafiki kati ya Seneti na Baraza la Kaunti Kisumu.

Murkomen, ambaye pia ni Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Seneti amejitosa Ijumaa kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter,  baada ya kuruhusiwa kwenda nyumbani, ambapo amewamiminia shukrani daktari aliyemtibu, wafuasi wake kwa kumwombea na Mola kwa uponyaji.

“Nilifanyiwa salama upasuaji wa kurekebisha viungo. Hatimaye nimeruhusiwa kurejea nyumbani. Namshukuru Prof Ating’a na timu yake. Ahsanteni kwa kunifariji na maombi yenu. Utukufu kwa Mungu aturejesheaye afya yetu na kuponya vidonda vyetu. Barikiweni,” aliandika.

Seneta huyo alianguka na kupata jeraha la bega lake la kulia mnamo Jumatatu jioni, wakati wa mchuano wa kirafiki wa soka katika uwanja wa maonyesho wa Ithookwe, Kitui.

Aliwahiwa katika hospitali ya Neema, Kitui na kisha kuhamishwa katika hospitali ya Nairobi.

Madaktari katika hospitali ya Nairobi walipendekeza afanyiwe upasuaji maalum kurekebisha bega lake, na kuibua hofu kuwa angekosa vikao vya seneti vya muda wa wiki moja vinavyoendelea katika Kaunti ya Kitui.

Kufuatia tukio hilo, wafuasi wake walijitosa mitandaoni wakimtakia afueni ya haraka.

Hata hivyo, baadhi walitumia masaibu ya wakili huyo kumkumbusha kutumia nafasi na mamlaka yake kubuni sheria zitakazosaidia kuboresha viwanja vya michezo nchini ambavyo vijana Wakenya hulazimika kutumia katika juhudi zao za kutuliza kiu chao cha spoti.