Habari Mseto

Seneta Mwaura aitikia kilio cha wahudumu wa tuktuk Githurai kuimarisha barabara mbovu

December 5th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

SIKU kadhaa baada ya wahudumu wa tuktuk Githurai kulalamikia hali mbovu ya barabara, hasa inayounganisha eneo hilo na mtaa wa Mwihoko, Kaunti ya Kiambu, kilio chao kimewafikia baadhi ya viongozi.

Chini ya muungano wa Tuktuk na magari madogo ya usafiri na uchukuzi aina ya Maruti, GTMA, juma lililopita, wahudumu hao walijituma kukarabati sehemu za barabara hiyo zilizosheheni mashimo.

Waliamua kuchukua hatua hiyo, huku wakitumia raslimali zao kununua mawe pamoja na kuyasafirisha, wakihoji malalamiko yao yameendelea kupuuzwa na viongozi waliochaguliwa eneo hilo.

Hata hivyo, Seneta maalum Isaac Mwaura ameungana na wahudumu hao kusaidia kuimarisha sehemu zilizotajwa kuathirika pakubwa.

Wahudumu wa tuktuk na Maruti wamekuwa wakiteta magari yao kuharibika kila wakati, kutokana na hali mbaya ya barabara.

Seneta Maalum, Isaac Mwaura (pili kutoka kulia juu katika lori) akipakua mawe aliyotoa kama msaada kusaidia kukarabati hali mbovu ya barabara Githurai. Picha/ Sammy Waweru

“Barabara eneo hili ni mbovu, na ndio maana nimeamua kuungana na watumizi hasa wendeshaji tuktuk kukarabati sehemu zilizoathirika pakubwa kwa kumwaga mawe niliyojitolea, kwenye mashimo,” Bw Mwaura akasema, akisikitikia hali mbovu ya barabara Githurai.

Seneta huyo na ambaye katika zoezi la mchujo wa uwaniaji wa kiti cha ubunge Ruiru, chini ya chama tawala cha Jubilee, Aprili 2017 alibwagwa na Simon King’ara (mbunge wa sasa Ruiru), alikuwa ameandamana na kikosi cha afisi yake Githurai 45 kukarabati barabara.

Githurai 45 ipo katika eneobunge la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

“Tunamshukuru Seneta Mwaura kwa kuitika kilio chetu. Kwa hakika tumekuwa tukikadiria hasara kila wakati kupeleka magari katika gereji kutengenezwa kwa sababu ya ubovu wa barabara. Isitoshe, hali iliyopo imekuwa ikichangia kuwepo kwa msongamano wa magari ambao huathiri Thika Road,” akaelezea Paul Kagiri, msimamizi wa nidhamu GTMA.

Bw Mwaura ameahidi kuendelea kuimarisha miundomsingi eneo hilo.