Habari Mseto

Seneta Naomi Jillo Waqo ajitetea

May 15th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA maalum Naomi Jillo Waqo ambaye ni mmoja wale ambao ilisemekana wataadhibiwa kwa kususia mkutano wa maseneta wa Jubilee uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi sasa anasema anaunga maamuzi yaliyofikiwa siku hiyo.

Kwenye taarifa aliyotoa Ijumaa, Bi Waqo amekariri uaminifu wake kwa kiongozi wa chama hicho Rais Uhuru Kenyatta akisema anaunga mkono amri zake zote.

Amesema alikosa kuhudhuria mkutano huo ulioongozwa na Rais kutokana na sababu zisizoepukika na ambazo “niliwaelezea kupitia barua kwa chama.”

“Kuhusu matukio ya kisiasa yanayoendelea katika chama chetu cha Jubilee, ningependa kusema kuwa uaminifu wangu ni kwa kiongozi wetu Rais Uhuru Kenyatta. Ninasimama na maamuzi yake kuhusiana na masuala yote kuhusu chama chetu na taifa la Kenya,” amesema.

Mnamo Jumanne Waqo ni miongoni mwa maseneta watano maalum ambao waliandikiwa barua wakitakiwa wafike mbele ya kamati ya nidhamu juma lijalo kuelezea ni kwa nini wasifurushwe kwa kukaidi mwaliko wa mkutano huo.

Wengine ni Bi Millicent Omanga, Bi Falhada Dekow Iman, Bw Victor Prengei na Mary Seneta.

Ni katika mkutano huo wa Ikulu uliohudhuriwa na maseneta 20 wa Jubilee na Kanu ambapo Seneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) alipokonywa wadhifa wake kama Kingozi wa Wengi na Susan Kihika (Nakuru) akavuliwa wadhifa wa Kiranja wa Wengi.

Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Caleb Kositany (Mbunge wa Soy) ameindikia chama hicho akihoji tishio la kuwaadhibiwa maseneta hao.

“Mbona masenta hao ndio wanalengwa kwa kuandikiwa barua ilhali maseneta wengine 22 hawakuhudhuria mkutano huo?” akauliza.

Bw Kositany amesema hatua ya kuwaadhibu maseneta hao sio ya haki kwa sababu mwaka 2019 baadhi ya wabunge wa Jubilee walikiuka msimamo wa chama kwa kumfanyia kampeni mgombeaji wa ODM katika uchaguzi mdogo wa Kibra.