Habari Mseto

Seneta Samson Cherargei akamatwa kuhojiwa DCI

December 3rd, 2019 1 min read

Na VINCENT ACHUKA

MAAFISA wa DCI wamemkamata Seneta wa Nandi, Samson Cherargei akidaiwa kutoa matamshi ya chuki na uchochezi huku akitarajiwa mahakamani baadaye.

Amekamatwa jijini Nairobi na amepelekwa katika makao makuu ya DCI, Kiambu Road, Nairobi kabla ya kufikishwa mahakamani.

“Seneta wa Nandi Samson Kiprotich Cherargei amekamatwa kuhusiana na matamshi ya chuki na uchochezi aliyotoa katika Shule ya Msingi ya Kilibwoni mnamo Agosti 17, 2019. Atafikishwa mahakamani kukabiliwa na mashtaka kwa kukiuka sehemu ya 96(a) ya taratibu za adhabu ya ukiukaji wa sheria,” imesema DCI.

Cherargei ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto katika video ya Agosti alidaiwa kuonya wapinzani wa Naibu Rais kwamba watachukuliwa hatua ambazo “hazibainiki”.

“Wanaomhujumu Ruto tunawaona; msidhani hana wafuasi,” akasema Cherargei.

 

Alikamatwa wakati huo lakini baadaye akaachiliwa.