Habari

Seneta Samson Cherargei akamatwa kwa kudaiwa kutoa matamshi ya uchochezi

August 20th, 2019 1 min read

Na WYCLIFFE KIPSANG na CHARLES WASONGA

SENETA wa Kaunti ya Nandi, Samson Cherargei amekamatwa na polisi Jumanne asubuhi nyumbani kwake katika mtaa wa Elgon View mjini Eldoret, Kaunti ya Uasin Gishu kwa madai ya kutoa matamshi ya uchochezi.

Maafisa kutoka Idara ya Upelelezi Jinai (DCI) walivamia nyumba ya mwanasiasa huyo mwendo wa saa moja za asubuhi na kumtia mbaroni.

Inadaiwa kuwa mnamo Jumamosi wiki jana, Bw Cherargei aliwashambulia wakosoaji wa Naibu Rais William Ruto kwa maneno yaliyofasiriwa kuwa vitisho, alipohutubu kwenye hafla ya mazishi katika eneo la Lessos, Kaunti ya Uasin Gishu.

Inadaiwa kwamba aliwaonya (wakosoaji wa Dkt Ruto) kwamba “sisi kama wafuasi wa Naibu Rais hatutanyamaza huku mkimtusi kila mara bila sababu. Tunawajua na tutapambana nanyi vikali wakati ukifika.”

Bw Cherargei ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Masuala ya Kikatiba na Haki, aliingizwa kwenye gari la polisi na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Eldoret Central.