Seneta taabani tena kwa dai la kujeruhi mwanamke

Seneta taabani tena kwa dai la kujeruhi mwanamke

KALUME KAZUNGU na JAMES MURIMI

SENETA wa Kaunti ya Lamu, Bw Anwar Loitiptip, amejipata taabani tena baada ya kudaiwa kumpiga risasi mwanamke mjini Nanyuki.

Afisa wa kitengo cha kuchunguza uhalifu katika Kaunti ya Laikipia, Bw Onesmus Towett, alithibitisha kuwa seneta huyo anachunguzwa kuhusiana na kisa hicho, kilichotokea usiku wa manane kuamkia jana. Bw Towett alisema seneta huyo, ambaye alipelekwa hospitalini Nairobi, aliambia polisi alikuwa ameshambuliwa na watu watatu ndipo akafyatua risasi.

“Anasema alikuwa akijilinda. Polisi wanafuatilia kisa hicho,” akasema.

Ripoti za polisi zilionyesha kuwa mwanamke aliyetambuliwa kama Bi Joy Makena, 32, alijeruhiwa kwa risasi katika mguu wake wa kulia.

Alipokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Nanyuki.

Kisa hiki kimetokea siku chache baada ya polisi wa Kaunti ya Lamu kuanzisha uchunguzi kuhusu madai kuwa, Bw Loitiptip alijaribu kumrusha mpinzani wake wa kisiasa baharini.

Bw Francis Mugo, 32, alijeruhiwa mkono wa kushoto katika kisa hicho kilichotokea ufuoni mwa bahari katika uwanja wa ndege wa Manda, Jumanne iliyopita. Hii ilikuwa muda mfupi baada ya Naibu Rais William Ruto kuondoka Lamu. Ilidaiwa pia Bw Loitptip alivunja miwani ya Bw Mugo na kumpokonya simu ya rununu.

Kamanda wa Polisi Lamu, Bw Moses Murithi, alithibitisha kupokea malalamishi hayo. Bw Mugo ni miongoni mwa vijana ambao wametangaza azma ya kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha useneta ifikapo Uchaguzi Mkuu wa 2022, akitarajia kupigania tiketi ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA).

“Nimehuzunishwa sana na tabia ya seneta wetu, Anwar Loitiptip kunipiga bila hatia na kujaribu kunitupa baharini. Ombi langu ni kwamba haki itendeke,” akasema Bw Mugo katika mahojiano na Taifa Leo.

Hata hivyo, Bw Loitiptip wakati huo alipuuzilia mbali malalamishi ya Bw Mugo na kudai kuwa nia yake ni kumharibia sifa.

Mnamo Juni, 2019, Bw Loitiptip alijeruhiwa vibaya kichwani pale alipopigwa na watu kadhaa kwenye baa moja jijini Nairobi.

Alidai kuwa, watu hao walimvamia alipokuwa akijaribu kumuokoa binti ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, Bi Saumu Mbuvi kutoka mikononi mwa mwanamume aliyedaiwa kumvamia chooni.

Iliripotiwa kuwa, baada ya Bw Loitiptip kumuokoa Bi Mbuvi, mwanamume huyo alitoweka kisha baadaye akarudi na wenzake, ambapo walimpiga kwa marungu Bw Loitiptip na kumwacha hoi sakafuni.

You can share this post!

ODM: Raila si ‘kifaranga’ wa serikali

Kiraitu atakiwa kulipa Sh274m kabla ya kukabidhiwa chama

T L