Habari Mseto

Seneta wa zamani ajinasua seli baada ya kulipa deni

December 14th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Seneta wa chama cha Jubilee Joy Gwendo aliyekuwa ameteuliwa kuwakilisha jinsia atasherehekea siku kuu ya Krismasi na shamra shamra za Mwaka Mpya wa 2019 akiwa huru baada ya kuachiliwa kutoka gereza la  Langata.

Bi Gwendo aliachiliwa na Jaji Ngenye Macharia wa Mahakama kuu ya Milimani Nairobi baada ya kuelezwa seneta huyo amelipa deni la Sh1.7 milion alilokuwa anadaiwa.

Kupitia kwa mawakili wake, Bi Gwendo, alimweleza Jaji Macharia kwamba mwanasiasa huyo amepinga adhabu iliyopitishwa dhidi yake na hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Bw Douglas Ogoti.

“Naomba hii mahakama imwachilie mfungwa huyu kutoka gereza kuu la wanawake la Lang’ata kaunti ya Nairobi,” Jaji Macharia aliombwa.

Mahakama ilifahamishwa tayari pesa alizokuwa amedaiwa kutumia vibaya zimelipwa.

Bi Gwendo alishtakiwa kwa kutumia mamlaka ya afisi yake vibaya kwa kujinufaisha na zaidi ya Sh2,2milioni zilizokuwa zimechangwa katika eneo la Kisumu Mashariki kuwafaidi wakulima wa pamba.

Shtaka dhidi ya Bi Gwendo lilisema mnamo Oktoba 23 2016 katika eneo la uwakilishi bungeni la Kisumu mashariki alijipatia Sh2,226,800 za chama cha ushirika cha wakulima wanaokuza pamba.

Pesa hizo zilikuwa zimechangishwa kupitia kwa vuguvugu la kustawisha wakazi wa eneo hilo la Kavali Development Initiative.

Ushahidi uliotolewa mbele ya Bw Ogoti ulisema kuwa Bi Gwendo alitumia mamlaka ya afisi yake kuwafilisi wakulima hao wa zao la pamba.

Bi Gwendo alikuwa ameomba fursa apewe muda wa kulipa deni hilo akisema “tayari nimelipa zaidi ya Sh500,000.”

Seneta huyo wa zamani alikuwa amemsihi Bw Ogoti mnamo Agosti 6, 2018.

Hakulipa kama alivyokuwa ameahidi..

Akipitisha hukumu  Bw Ogoti alisema “….Ni bayana kuwa mshtakiwa alidai atalipa deni hili kwa vile amesikizana na afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) ndipo aondolewe kesi.”

Akasema Bw Ogoti, “Mshtakiwa alikuwa anafanyia mahakama mzaha. Alijua hatalipa. Alidanganya mahakama.”

Mahakama ilimpata na hatia Bi Gwendo na kumsukumia kifungo cha miaka miwili bila faini.