Siasa

Seneta Wamatinga awataka viongozi Mlimani kudandia ‘basi’ moja

January 23rd, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

SENETA wa Nyeri Wahome Wamatinga amesema ingekuwa vyema viongozi kutoka Mlima Kenya kushabikia vyama vyenye mizizi katika eneo hilo.

Bw Wamatinga alisema malumbano ya kisiasa yanayoshuhudiwa huko yangeepukika kama kosa hilo lingeepukwa kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Kwa sasa, Bw Wamatinga anasema kuwa huenda ukosefu wa chama kimoja ndio umechangia malumbano yanayoshuhudiwa kwa sasa baina ya viongozi tofauti katika eneo hilo.

Mnamo Jumatatu, Bw Wamatinga alisema kwamba ijapokuwa eneo hilo lilipigia kura kwa wingi chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA), ingekuwa bora ikiwa lingekuwa na chama chake cha kisiasa, kama maeneo mengine nchini.

“Kama jamii, ni vizuri kuwa na chama kunachotuunganisha; chama ambacho ni kama mwamvuli wetu wa kisiasa unaontusaidia kuzungumza kwa sauti moja. Ushauri wangu ni kuwa ikielekea 2027, eneo hili linafaa kuwa na chama kinacholipa utambulisho wa kisiasa,” akasema Bw Wamatinga kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio.

Kauli yake inafuatia ubabe wa kisiasa ambao umekuwa ukishuhudiwa baina na Naibu Rais Rigathi Gachagua na mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu).

Kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022, eneo hilo lilikipigia kura kwa wingi chama cha UDA, kilicho katika mrengo wa Kenya Kwanza.

Katika siku za hivi karibuni, baadhi ya viongozi katika eneo hilo wamekuwa wakilalamikia “kutengwa” kwenye masuala yanayohusu uendeshaji wa shughuli muhimu za chama hicho.

Baadhi ya viongozi ambao wamejitokeza wazi kutoa kauli kama hizo n Gavana Mutahi Kahiga wa Kaunti ya Nyeri.

Hata hivyo, Bw Wamatinga alisema uwepo wa chama kimoja cha kisiasa utarejesha umoja wa kisiasa uliokuwepo katika eneo hilo, kama enzi za marais wastaafu hayati Mzee Jomo Kenyatta, (marehemu) Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta.

“Wakati wa viongozi hao, eneo hili lilikuwa chini ya vyama kama Democratic Party (DP), The National Alliance (TNA) kati ya vingine vingi,” akasema seneta huyo.