Habari Mseto

Seneti kuandaa vikao vyake Kitui mnamo Septemba

June 18th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Seneti litaendesha vikao vyake nje ya Nairobi, kwa mara ya pili mwaka 2019, katika Kaunti ya Kitui kuanzia Septemba 16 hadi 20.

Vikao hivyo vitaendeshwa katika majengo ya Bunge la Kaunti ya Kitui ambapo hoja na miswada kadhaa itajadiliwa.

Maseneta hao 67 pia watatumia nafasi hiyo kushughulikia masuala yanayowahusu wakazi wa kaunti hiyo ya Kitui inayowakilishwa na Seneta Enock Wambua.

Seneti iliandaa vikao vyake nje ya Nairobi katika kaunti ya Uasin Gishu mnamo Septemba mwaka jana.

Alhamisi wiki jana, maseneta walipitisha kwa kauli moja hoja iliyowasilishwa na kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen iliyopendekeza kuwa vikao hivyo viandaliwe katika kaunti ya Kitui.

Bw Murkomen ambaye ni Seneta wa Elgeyo Marakwet alisema uamuzi wa Maseneta kuandaa vikao nje ya Nairobi unafungamana na sheria za bunge hilo na Katiba.

“Katiba na Sheria za Bunge la Seneti zinairuhusu Seneti au Bunge la Kitaifa kuandaa vikao nje ya Nairobi,” akasema.

Bw Murkomen aliongeza kuwa Kamati za Seneti pia zinaendesha vikao katika Majengo ya Bunge la Kaunti ya Kitui jinsi inavyofanyika katika majengo ya bunge, Nairobi.

“Na wakazi wa Kitui pamoja na wageni wengine watakuwa huru kuhudhuria vikao vya Kamati za Seneti na hata Kamati za Bunge lote, mradi wanazingatia taratibu zilizowekwa,” akasema Bw Murkomen.

“Vikao hivi bila shaka vitawapa wakazi wa Kitui fursa ya kutangamana moja kwa moja na maseneta katika moyo wa ushirikishwaji wa umma katika shughuli za utayarishaji wa sheria,” akaongeza.

Spika kuongoza vikao

Spika wa Seneti Ken Lusaka alisema ataongoza vikao vya kamati ya bunge lote kama ambavyo amekuwa akifanya katika majengo ya Bunge Nairobi.

“Hatua ya kuandaa vikao vya seneti katika ngazi ya kaunti inalenga kuwapa maafisa wa mabunge ya kaunti na umma kwa jumla nafasi ya kujifunza kutokana na namna shughuli huendeshwa katika bunge la seneti,” akasema Bw Lusaka.

Vikao hivyo pia vitawawezesha wananchi kuelewa wajiibu wa seneti kando na kushirikishwa kwao katika kazi ya bunge hilo, akaongeza Bw Lusaka.

Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alisema kuandaliwa kwa vikao vya seneti katika kaunti ya Kitui pia kutatoa fursa kwa madiwani wa kaunti hiyo kuelewa utendakazi wa Seneti.

“Hasa wataelewa wajibu wetu wa kikatiba wa kulinda ugatuzi na matumizi ya pesa za umma. Wataelewa zaidi sababu inayosababisha seneti kualika magavana kujibu maswali yaliyoibuliwa kwenye ripoti za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali Edward Ouko kuhusu matumizi ya fedha katika kaunti hiyo,” akasema Bw Ledama.

Kiongozi wa wachache James Orengo naye alisema kwa kwenda mashinani, maseneta watakuwa wakitekeleza sawasawa wajibu wao wa uwakilishi.

“Tukienda Kitui tutathibitisha kuwa tunajali kuhusu yale yanayotendeka mashinani zaidi pengine hata kuliko hapa Nairobi. Kazi yetu ya uwakilishi wa wapigakura utakuwa umekamilika,” akaongeza Bw Orengo ambaye ni Seneta wa Siaya.