Habari

Seneti kuchunguza kifo cha Walibora

April 25th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Seneti Jumatatu litaanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha mwandishi hodari na mwanahabari marehemu Profesa Ken Walibora.

Kamati ya Seneti kuhusu Afya imemwagiza Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali Kuu ya Kenyatta (KNH) Dkt Evans Kamuri kujibu maswali kuhusu madai kuwa Walibora alitelekezwa na wahudumu wa hospitali hiyo alipowahiwa huko baada ya kugongwa na matatu.

Kamati ya Seneti kuhusu Afya inayoongozwa na Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito inafuatilia ripoti kwamba marehemu Profesa Ken Walibora alifariki baada ya kutelekezwa katika kitengo cha kuwapokea majeruhi cha KNH.

“Kamati hiyo imemwagiza Afisa Mkuu Mtendaji wa hospitali hiyo kufika mbele yake Jumatatu, Aprili 27, 2020, ili aeleze kilichotokea katika kitengo cha majeruhi cha hospitali hiyo huku uchunguzi wa kifo hicho ukianza,” Seneti ikasema Ijumaa kupitia ukurasa wa akaunti ya Twitter.

Kando na Dkt Mbito, wanachama wengine wa kamati hiyo ni; Abdullahi Ibrahim (Wajir), Beth Mugo (Seneta Maalum), John Kinyua (Laikipia), Falhada Iman (Seneta Maaulum) Eric Mogeni (Nyamira), Petronilla Lokorio (Seneta Maaulum), Naomi Masitsa (Seneta Maaulum) na Fred Outa (Kisumu).

Profesa Walibora ambaye ni mwandishi wa riwaya maarufu ya ‘Siku Njema’ miongoni mwa kazi zingine za fasihi alifariki mnamo Ijumaa, Aprili 10, 2020, baada ya kugonjwa na matatu katika barabara ya Landhies, Nairobi.

Polisi wanachunguza chanzo cha kifo chake baada ya mpasuaji mkuu wa maiti aliye chini ya ajira ya serikali Johannsen Oduor kugundua kuwa kando na majeraha ya kugongwa na gari alidungwa na kifaa chenye makali kama ya kisu katika mkono wake wa kulia.

Baadhi ya watu waliokuwepo pahala pa mkasa waliwaambia wanahabari wa runinga kwamba marehemu alikuwa akikimbizwa na watu fulani na ndipo akagongwa na matatu akivuka barabara ya Landhies.

Walibora alizikwa Jumatano nyumbani kwao katika kijiji cha Huruma, Makutano, eneobunge la Cherangany, Kaunti ya Trans Nzoia.