Habari MsetoSiasa

Seneti kuita mabunge ya kaunti kueleza yanavyotumia pesa

July 17th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

SENETI inapanga kuanza kuwaweka madiwani katika kibarua kueleza jinsi wanatumia pesa wanazopewa na serikali za kaunti, katika mabadiliko ya mambo kwani hawajakuwa wakihitajika kuwajibika.

Kamati ya Bunge la Seneti kuhusu Ukaguzi wa Matumizi ya Pesa za Kaunti Jumanne ilisema kuwa kuanzia Oktoba itaalika mabunge ya kaunti mbele yake, kueleza jinsi yamekuwa yakitumia pesa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Moses Kajwang (pichani) alisema japo mabunge hupokea mgao wa pesa za kaunti, mengi yao yamekuwa yakiripotiwa kuzitumia isivyofaa, hivyo yakihitajika kuwajibika.

“Miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba tutaalika mabunge ya kaunti kuzungumza nayo. Kuna asilimia 12.5 ya pesa za kaunti ambazo huenda kwa mabunge hayo, ambazo tunafaa kufahamu jinsi zinavyotumiwa,” akasema Bw Kajwang.

Bw Kajwang, ambaye pia ni seneta wa Homa Bay alisema sharti mabunge hayo yaeleze taifa jinsi yamekuwa yakitumia pesa, kwani ni pesa za walipa ushuru.

“Tunataka mabunge hayo yatoe mwanga kwa taifa jinsi pesa hizo zinatumiwa,” akasema.

Mbali na hayo, alisema kamati hiyo itaanza kuzunguka katika kaunti tofauti kujionea jinsi kazi na shughuli za maendeleo zinaendelezwa, akisema ni vyema kujionea ikiwa ugatuzi unaleta tofauti.

“Vilevile, tutajipeleka katika kaunti tofauti kushuhudia moja kwa moja jinsi pesa za wananchi zinatumiwa,” akasema.