Habari Mseto

SENETI: Mambo bado

September 8th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KWA mara nyingine Seneti Jumanne iliamua kuahirisha mjadala kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti hadi wiki ijayo baada ya maseneta kukosa kupata muafaka kuhusu suala hilo.

Japo Spika Kenneth Lusaka alisema hatua hiyo ililenga kutoa nafasi ya mazungumzo zaidi, maseneta tuliozungumza nao walisema kuwa waliafikiana kuahirisha mjadala huo ili wapate nafasi ya kupitisha mswada utakaoiruhusu Hazina ya Kitaifa kusambaza asilimia 50 ya fedha kwa serikali za kaunti.

Kiranja wa wengi katika Seneti Irungu Kang’ata alisema kuwa bunge hilo litaupa mswada huo wa marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, kipaumbele kama njia ya kuziondolea kaunti changamoto za fedha zinazozisibu wakati huu.

“Mswada huu utashughulikiwa katika hatua ya pili na ya tatu kabla ya kupitishwa wiki ujao,” Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a akaeleza.

Mswada huo, ambao ulipitishwa katika Bunge la Kitaifa Novemba mwaka jana, unatoa nafasi kwa Hazina ya Kitaifa kusambaza hadi asilimia 50 ya mgao wa fedha wa mwaka uliotangulia endapo Mswada wa Ugavi wa Mapato (DORA) utachelewa kupitishwa.

Hata hivyo, Bw Kang’ata alisema maseneta sasa wataufanyia marekebisho kwa kuingiza kipengele kinachotoa nafasi kwa Hazina ya Kitaifa kusambaza asilimia 50 ya fedha kwa serikali endapo kupitishwa kwa Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti (CARB) kutecheleweshwa, ilivyo sasa.

“Ni maseneta wamekubali kupitisha mswada huu haraka, baada ya kuufanyia marekebisho kwa kujumuisha mswada wa CARB. Kazi hii tutaimaliza kufikia wiki kesho na hatua ambayo itatoa nafasi kwa serikali za kaunti kupokea fedha za kufadhili shughuli za kila siku na kuwalipisha wafanyakazi mishahara,” akasema Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a.

Mswada huo uliwasilishwa kwa Seneti mnamo Novemba 18, 2019, baada ya kupitishwa katika bunge la kitaifa, ili ujadiliwe na upitishwe, lakini maseneta hawakuushughulikia.

Mswada huo uliodhamini na Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichung’wa baada ya Seneti na Bunge la Kitaifa chelewesha kupitishwa kwa mswada wa DORA kwa miezi mitatu mwaka 2019 na kuzikosesha serikali za kaunti fedha.W

Wabunge walishikilia kuwa serikali za kaunti zitengewe Sh316.5 bilioni pekee kutoka Hazina ya Kitaifa lakini maseneta wakipendekeza Sh335 bilioni. Baadaye maseneta walisalimu amri na kukubaliana na pendekezo la wabunge, japo kwa shindo upande.

Jana, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alisema kuwa ameafikiana na Bw Lusaka kwamba mswada huo ushughulikiwe kwa haraka katika Seneti.

“Vile vile, nimeagiza kiongozi wa wengi Amos Kimunya kushirikiana na mwenzake wa Seneti Samuel Poghisio ili wahakikishe kuwa mswada huo umepitishwa na marekebisho yatakayotoa nafasi kwa kaunti kupokea asilimia 50 ya mgao wa fedha,” akasema.

Mwenyekiti wa baraza la magavana Wycliffe Oparanya ametisha kwamba serikali za kaunti zitasitisha shughuli mnamo Septemba 17 ikiwa maseneta hawatakuwa wametanzua mvutano huo.