Habari Mseto

Seneti yaambiwa raia 210 waliuawa na polisi

March 5th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

JUMLA ya raia 210 wameuawa na polisi kinyume cha sheria katika kipindi cha miezi 15 iliyopita, hii ni kwa mujibu wa Mamlaka ya Kuchunguza Utendakazi wa Maafisa wa Polisi nchini (IPOA).

Mwenyekiti wa mamlaka hiyo, Bi Anne Makori jana aliwaambia maseneta kwamba kati ya watu hao, 146 walipigwa risasi hadharani na polisi, 39 walifariki katika vituo vya polisi huku 25 wakipatikana wamefariki baada ya kutekwa nyara na polisi.

Bi Makori aliambia wanachama wa Kamati ya Seneti kuhusu Masuala ya Sheria na Haki na Kibinadamu kwamba asasi hiyo imekamilisha uchunguzi kuhusu visa 110 na kuwasilisha faili hizo kwa Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) Noordin Haji ili watuhumiwa wafunguliwe mashtaka.

“Kati ya faili hizo, 75 zimewasilishwa mahakamani na zingine 35 zingali zinashughulikiwa katika afisi ya DPP.

“Vilevile, kuna visa vingine 20 ambavyo tulikamilisha kuchunguza wiki jana na tunatarajia kuwasilisha faili zao kwa afisi hiyo,” akawaambia wanachama wa kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Seneta wa Nandi, Bw Samson Cherargei.

Baadhi ya visa ambavyo IPOA imekamilisha kuchunguza ni mauaji ya mauaji ya mvulana mwenye umri wa miaka mitatu, Dancan Githinji, katika kijiji cha Soweto, mtaa wa Kahawa West, Nairobi, mnamo Novemba 8, 2019.

Kisa kingine ni mauaji ya Bw Carliton Maina katika eneobunge la Kibra, Nairobi mnamo Desemba 22, 2018 ambapo polisi mhusika anasubiri kuwasilishwa kortini kukabiliwa na mashtaki ya mauaji kwa kukusudia.

Vilevile, IPOA imekamilisha uchunguzi wa kisa ambapo polisi walimpiga risasi na kumuua Ahmed Majid mnamo Januari 16, 2020 katika eneobunge la Kamukunji, Nairobi.

Bi Makori aliwaambia maseneta hao kwamba katika kipindi hicho cha miezi 15, maafisa sita wa polisi wamepatikana na hatua ya kutekeleza mauaji ya raia kiholela na kuhukumiwa.

“Watatu kati yao wamepewa adhabu ya kifo,” akasema akiongeza kuwa hiyo ni ishara kwamba IPOA inatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria.

Bi Makori alikuwa amefika mbele ya Kamati hiyo pamoja na makundi kadhaa ya kutetea haki za kibinadamu kuangazia hatua ambazo zimechukuliwa na wadau mbalimbali kudhibiti kero hilo.

Miongoni mwa mashirika yaliyohudhuria kikao cha kamati hiyo katika ukumbi wa County, Nairobi ni Amnesty International (AI), Haki Afrika, International Medico- Legal Unit, na Social and Justice Centre.

Mashirika hayo yaliitaka Seneti ipendekeze kuundwe kwa tume ya kisheria ya kuchunguza visa vya mauaji yanayotekelezwa na polisi kinyume cha sheria.