Habari

Seneti yaamuru EACC kuchunguza sakata ya uuzaji kipande cha ardhi mahususi kwa mradi wa maji Kericho

November 21st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Seneti limeamuru Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuchunguza kubaini iwapo sheria ilikiukwa serikali ya Kaunti ya Kericho iliponunua ekari 10 ya ardhi kwa ajili ya ujenzi mradi wa maji Kimugu.

Hii ni baada ya ripoti ya mkaguzi wa hesabu za serikali kuibua maswali kuhusu ununuzi wa ardhi hiyo kutoka kwa kampuni ya kuendesha kilimo cha majanichai ya Unilever Tea Company.

Kulingana na ripoti hiyo iliyotiwa saini na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aliyeondoka ofisini Edward Ouko, ardhi hiyo haikuwa mali ya kampuni hiyo, mapema mwaka 2019 wakati ambapo iliuzia serikali ya Kaunti ya Kericho kwa Sh103 milioni.

“Ardhi hiyo ya ekari 10 iliyonunuliwa na serikali ya Kericho kwa ajili ya ujenzi wa mradi ya maji ilikuwa ni ardhi ya umma wakati ambapo kampuni ya Unilever Tea iliuza. Hii ni kwa sababu ardhi hiyo imekuwa chini ya usimamizi wa iliyokuwa manisipaa ya Kericho kwa zaidi ya miaka 12. Kwa hivyo, ardhi hiyo inafaa kuwa mojawapo ya mali ambayo serikali ya Kaunti ya Kericho ilirithi kutoka kwa manisipaa hiyo,” ikasema ripoti hiyo ya mwaka wa kifedha wa 2017/2019.

Kulingana na ripoti hiyo ambayo ilichambuliwa na kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu wa Pesa za Umma na Uwekezaji (CPAIC) Jumanne, Kaunti ya Kericho ilinunua ardhi hiyo kwa bei ya juu kupita kiasi.

“Kwa kuwa serikali ya Kericho ilinunua ardhi hiyo kwa Sh103 milioni ina maana kuwa ekari moja ya ardhi iliuzwa kwa zaidi ya Sh10 milioni. Bei hii ni ya juu zaidi ikizingatiwa kuwa huu ni mradi wa umma,” akasema Seneta wa Narok Ladema Ole Kina.

“Hapa kuna ufisadi. Inaoenekana kuwa kuna maafisa wa serikali ya kaunti ya Kericho walioshirikiliana na Unilever kuipunja serikali ya kaunti hii. Suala hili linapasa kuchunguzwa na EACC,” akasema Seneta huyo wa ODM.

Kauli yake iliungwa mkono na mwenyekiti wa Kamati hiyo Moses Kajwang’ ambaye alisema EACC pia inapasa kuchunguza sababu ilipelekea serikali ya kaunti ya Kericho kununua “ardhi ya umma kutoka kwa kampuni ya kibinafsi”

“Hii ni sakata inayofanana na ile ya ununuzi wa ardhi ya Ruaraka ambapo kamati hii ilichunguza na kubaini kuwa serikali ililaghaiwa kununua ardhi ya umma. Iweje, serikali ya Kaunti ya Kericho iuziwe ardhi ambao kisheria, ni ardhi ya umma. Mbona inunue ardhi ya kuanzishia mradi wa umma kwa bei ya juu kiasi hicho? EACC ichunguze sakata hii kwa lengo la kuwashtaki wahusika wote,” akasema Bw Kajwang’ ambaye ni Seneta wa Kaunti ya Homa Bay.

Mradi huo unaojulikana kama Kimugu Water Treatment Plant uko katika eneo la Duka Moja kando ya barabara kuu ya Kericho-Nakuru.

Gavana wa Kericho Profesa Paul Chepkwony ambaye alifika mbele ya kamati hiyo ya CPAIC alikubaliana na maseneta kwamba serikali yake iliuziwa ardhi hiyo kwa bei ya juu kupita kiasi.

“Nakubaliana na kauli yenu waheshimiwa maseneta kwamba hii bei ya Sh10 milioni kwa ekari moja ni juu zaidi. Bei ya kawaida ya ardhi katika eneo la Duka Moja ni kati ya Sh2 milioni hadi Sh4 milioni kwa ekari. Lakini tulikubali bei ya Sh10 milioni kwa sababu haja yetu kuu ilikuwa ni kuzima changamoto ya muda mrefu ya maji katika Kaunti ya Kericho,” akasema Profesa Chepkwony.

Gavana huyo alisema mradi huo, ambao ujenzi wake utagharimu Sh1.18 bilioni, unalenga kutoa maji kwa zaidi ya wakazi 200,000 wa Kaunti ya Kericho utakapokamilika.