Habari Mseto

Seneti yaanza kupiga darubini hatima ya Waiguru

June 23rd, 2020 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

WAWAKILISHI wa wadi katika Bunge la Kaunti ya Kirinyaga Jumanne wamesisitiza kuwa liwe liwalo hawatawahi kumkumbatia Anne Mumbi Waiguru kama gavana wao.

Wamesema kuwa ikiwa Waiguru ataponyoka shoka la kung’atuliwa na bunge hilo katika seneti, basi ajiandae kurejea Kirinyaga kupambana na ung’atuzi mwingine.

“Sheria inatupa miezi mitatu ya mapumziko kabla ya kuandaa hoja nyingine ya kumng’atua Bi Waiguru. Ikiwa ataponyoka shoka hili Nairobi, hapa Kirinyaga hatapata pa kujificha,” amesema Kinyua Wa Wangui kutoka wadi ya Mutira, mwandalizi wa mswada uliomng’atua Waiguru kwa kura 23 kati ya 33 na ambapo nne hazikupigwa. Madiwani sita walikosa kujitokeza bungeni kufanya maamuzi.

Waiguru anatarajiwa kujitetea mbele ya bunge la Seneti hapo kesho Jumatano.

Madiwani hao waliomng’atua wamefika mbele ya bunge hilo la seneti leo Jumanne kuwasilisha ushahidi wao dhidi ya gavana wao.

Bw Wangui alisema kuwa katika kipindi kilichosalia cha utawala wa Gavana Waiguru, kuna hadi fursa tisa za kumng’atua.

“Akirejeshwa na Seneti, tunamng’atua na hiyo ndiyo itakuwa desturi hadi awamu yake itamatike. Kamwe hatutavumilia utumiaji mbaya wa nafasi za kiutawala na ukosefu wa maadili na heshima za kimsingi kutoka kwa huyu gavana wetu ambaye kwa sasa ni mshukiwa mbele ya haki ya bunge la Seneti na la Kirinyaga,” akasema.

Kiranja wa wengi katika bunge la kaunti ya Kirinyaga, Kamau Murango kutoka wadi ya Kerugoya alisema kuwa “kila ung’atuzi dhidi ya Waiguru kwa hadi mara tisa, utakuwa ukizingatia maovu tofauti ya kiutawala.

“Makosa ya Waiguru ni mengi kiasi kwamba hata ikibidi, kumng’atua mara 10 zaidi kutakuwa kwa msingi wa maovu mapya kabisa yasiyo na uhusiano wowote na ya awali. Ukora wa utawala wake umekita mizizi hapa mashinani kiasi kwamba huwezi ukakusanya wote kwa kapu moja kushughulikia ung’atuzi mmoja…” akadai.

Naye wakili wa bunge hilo la kaunti Ndegwa Njiru alisema kwamba mkondo wa sheria unafaa ufuatwe hadi ukingoni mwake ili kubaini hasa mwelekeo wa Seneti na uhalali wa maamuzi yake.

“Ni vyema tungojee mkondo wote utamatike ndipo tuwe na masuala ya kurejelea kuhusu uhalali na umakinifu ndani ya busara au ukosefu wayo kwa bunge la seneti. Tutajitokeza kutoa ushahidi wetu na kila atakayefuatilia ataelewa kama tumemakinikia suala hili au la. Tutakuwa na nafasi ya kufanya maamuzi yetu kuhusu jinsi seneti itakavyoamua. Kwa sasa naomba subira na tukome hisia kali kabla ya kushuhudia matokeo,” akasema.

Upande wa Waiguru nao ukisema umejiandaa kwa kesi hiyo ambayo itasikizwa na maseneta 11 kinyume na matarajio ya wengi Kirinyaga ambao walikuwa wakipendelea asikizwe na safu nzima ya seneti.

Hatua hiyo ya kumweka kwa maseneta 11 imetajwa na wengi kuwa ya kumpa Waiguriu wakati rahisi wa kuwashawishi kwa maneno na ufadhili maseneta hao huku kiranja wa wengi Irungu Kang’ata tayari akiwa sakafuni akijitetea dhidi ya madai kwamba alipokezwa Sh27 milioni kama “chai ya maseneta kufaa uokozi wa Bi Waiguru.”

Kang’ata aliambia Taifa Leo kuwa “hizo ni propaganda za kisiasa na kamwe sijapokea mlungula huo na mimi sina ushawishi wa maamuzi ya maseneta wote bali nazingatia tu masuala ya chama cha Jubilee.”