Seneti yaanza kusikiliza mashtaka ya kumtimua Trump

Seneti yaanza kusikiliza mashtaka ya kumtimua Trump

Na AFP

SENETI ilianza kusikiliza mashtaka yanayonuia kumuondoa mamlakani Rais Donald Trump huku maseneta wakisisitiza kutoonyesha upendeleo katika uamuzi wao.

Kwa mara ya tatu katika historia ya Amerika, seneti ilibadilishwa kuwa mahakama ya kusikiliza ombi la kumtimua rais, chini ya usimamizi wa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Juu John Roberts, ambaye aliwalisha kiapo maseneta hao.

Roberts alipowauliza iwapo waliapa kutoa haki bila mapendeleo kulingana na katiba ya Amerika, maseneta 99 – mmoja hakuhudhuria- walijibu kwa pamoja “ ndio” huku wakiinua mikono yao ya kulia.

Mapema Alhamisi, mashtaka mawili dhidi ya Trump yalisomwa kwenye seneti. Bunge la Congress linataka rais huyo kupatikana na hatia ya kutumia vibaya mamlaka yake na kuzuia bunge kutekeleza majukumu yake.

Adam Schiff, mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu ujasusi ataongoza mashtaka. Trump amekuwa akijeli mashtaka hayo na alitaja kuanza kusikilizwa kwa ombi kama mzaha.

“Nafikiri inapaswa kuharakishwa,” Trump aliambia wanahabari katika Oval Office.

“Ni ya ubaguzi. Nimepitia mzaha ulioendelezwa na Democrats ili waweze kujaribu na kushinda uchaguzi.”

Bunge la Congress lililo na wanachama wengi wa chama cha Democrats walipitisha hoja ya kumtimua Trump mamlakani Desemba 18.

Hata hivyo, Trump anatarajiwa kunusurika katika seneti iliyo na wanachama wengi wa chama chake cha Republican. Inahitaji hoja kuidhinishwa na thuluthi mbili ya maseneta ili kumuondoa rais mamlakani.

Baada ya kula kiapo, maseneta waliharisha kikao hadi Jumanne ijayo.

Seneta mmoja wa Republican – James Inhofe – hakuhudhuria kikao cha Alhamisi lakini alisema atakula kiapo Jumanne.

Trump analaumiwa kwa kuchelewesha msaada wa kijeshi kwa Ukraine na maafisa wa Ikulu ya White House kukutana na rais wa nchi hiyo ili kumpata habari kuhusu mpinzani wake wa kiti cha urais wa chama cha Democrat Joe Biden.

Bunge iliamua kuwa Trump alikiuka sheria kwa kuchelewesha msaada wa pesa uliopitishwa na wabunge kwa Ukraine.

Shtaka la pili linalolenga kumuondoa ofisini ni la kukataa kutoa mashahidi na stakabadhi kwa wachunguzi wa bunge.

Kiongozi wa wengi katika seneti Mitch McConnell amekuwa akikosoa hatua ya bunge ya kumtimua Trump na wabunge wa Democratic wanamlaumu kwa kupanga kuvuruga mashtaka hayo yatakapokuwa yakisikilizwa.

Alisema ataongoza seneti kumtetea Trump.

“Wakati wa bunge umeisha,” alisema McConnell “ sasa ni wakati wa seneti,” alisisitiza.

Spika wa bunge Nancy Pelosi alisema hatua ya Trump ilihujumu usalama wa taifa, ilikiuka kiapo cha ofisi yake na kuhatarisha uadilifu wa uchaguzi.

You can share this post!

Mahakama yazima uteuzi wa Wambui kusimamia uajiri

Rais Kenyatta atangaza mikakati mipya ya kupambana na...

adminleo