Habari MsetoSiasa

Seneti yaishtaki Bunge la Kitaifa

July 18th, 2019 2 min read

Na Richard Munguti

MTAFARUKU na malumbano makali ya utunzi na upitishaji sheria na mabunge mawili umepelekwa kwa Jaji Mkuu (CJ) David Maraga kuteua jopo la majaji watatu kuamua masuala tata na nyeti yanayozua cheche za maneno na chuki.

Katika kesi hiyo Bunge la Seneti linapinga sheria iliyopitishwa ya makadirio ya matumizi ya zaidi ya Sh3.02trilioni za bajeti ikisema “haikuichangia ipasavyo kisheria.”

Sheria nyingine inayolengwa ni Sheria ya Afya jinsi ya kuthibiti ununuzi wa dawa zinazotumika katika hospitali za umma (Kemsa), usimamizi wa mamlaka ya taasisi za kutoa mafunzo ya tiba za afya (MTCs) miongoni mwa sheria nyingine.

Kesi hiyo iliwasilishwa mbele Jaji Weldon Korir aliyeiratibisha kuwa ya dharura.

Maseneta 67 wakipinga sheria 24 zilizopitishwa na bunge la kitaifa wanasema tabia hii ya bunge la kitaifa imesababisha mzozo mkali kati ya mabunge haya.

Jaji Korir alisema katika uamuzi wake kuwa masuala tata na nyeti yanaimbuliwa katika kesi hiyo na “ yanahitaji kushughulikiwa kwa pupa na kuamuliwa ndipo wananchi wasiathiriwe.”

Jaji Korir alisema kesi hiyo iko na umuhimu kwa umma ikitiliwa maanani mabunge ya kaunti yanakumbwa na mizozo mikali ya kifedha.

Baraza la Magavana (CoG) waliwasilisha kesi katika Mahakama ya Juu wakisema mgawo wa pesa waliotengewa na bunge la kitaifa hautoshi kugharamia mahitaji ya magatuzi.

CoG inaomba mgawo huo uongezwe kutoka Sh310bilioni hadi Sh335bn.

Wakiongozwa na Spika wa Seneti Keneth Lusaka ,maseneta hao 67 waliwasilisha kesi wakiomba kufutiliwa mbali sheria 24 zilizopitishwa na bunge pasipo na mchango wao.

Maseneta mawakili James Orengo , Mutula Kilonzo Junior, Okong’o Omogen, Moses Wetang’ula , Kipchumba Murkomen na Kithure Kindiki walimweleza Jaji Korir kwamba “ bunge la kitaifa limekaidi na kukandamiza sheria kwa kutopeleka sheria inazotunga kupigwa msasa kabla ya kuidhinishwa kirasmi.”

“Kuna sheria 24 ambazo zilipitishwa na bunge la kitaifa bila mchango wa bunge la Seneti inavyotakiwa kisheria,” Jaji Korir alifahamishwa na Bw Orengo.

Katika kesi iliyowasilishwa mbele ya Jaji Korir, bunge la Seneti limeishtaki Bunge la Kitaifa na Mwanasheria Mkuu. Baraza la Magavana limetajwa katika kesi hiyo kuwa mhathiriwa na maagizo yatakayotolewa.

Bunge la Seneti linaomba mahakama kuu ifutilie mbali sheria 24 zilizotungwa na kupitishwa na bunge pasi na mchango wake.

“ Sheria iko bayana kwamba bunge la kitaifa likitunga sheria lapasa kuziwasilisha kwa Seneti kupigwa msasa na kuidhinishwa kabla ya kupitishwa kuwa sheria,” Bw Orengo alimweleza Jaji Korir.

Wakili huyo mwenye tajriba ya juu aliieleza mahakama kuwa bunge la kitaifa chini ya uelekezi wa kiongozi wa walio wengi Bw Aden Duale imevunja na kukiuka sheria katika utenda kazi wake.

“ Bunge la kitaifa lajukumiwa na katiba na sheria kushirikiana na bunge la Seneti katika utenda kazi wake,” alisema Bw Orengo akiongeza , “ Ni hii mahakama tu inayoweza kuikosoa na kuirekebisha bunge.”

Jaji Korir aliwaagiza maseneta hao wakabidhi mwanasheria mkuu na bunge la kitaifa nakala za kesi hiyo wajibu.

Kesi itatajwa Julai 26, 2019.