Seneti yaondolea KNH lawama kuhusu kifo cha Walibora mauko yake yakisalia kitendawili

Seneti yaondolea KNH lawama kuhusu kifo cha Walibora mauko yake yakisalia kitendawili

Na CHARLES WASONGA

SIKU 10 baada ya familia, jamaa, marafiki na mashabiki wa mwandishi mashuhuri marehemu Ken Walibora kuadhimisha mwaka mmoja baada ya kifo chake, maseneta wameondolea Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) lawama kuhusu kifo chake.

Kwenye ripoti yake ya uchunguzi kuhusu kiini cha kifo cha mwandishi huyo, Kamati ya Seneti kuhusu Afya inasema haikuweza kuthibitisha kuwa Walibora alifariki kutokana na “utepetevu wa KNH”.

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Trans-Nzoia, inasema kuwa marehemu Walibora alipokea huduma za kimatibabu hitajika alipofikishwa KNH “baada ya kugongwa na gari katika barabara ya Landhies, Nairobi, mnamo Aprili 10, 2020.”

“Alipewa huduma za dharura katika kitengo cha kuwahudumia wagonjwa mahututi katika idara ya kuwahudumia majeruhi wa ajali,” sehemu ya ripoti hiyo ikasema.

Maseneta pia wanasema kuwa marehemu Walibora ambaye alikuwa mwanahabari mtajika, aliandikishwa KNH kama “Mwanamume Mwafrika asiyejulikana” kwa sababu stakabadhi za kumtambua hazikupatikana.

“Marehemu alisalia hospitalini kwa siku tatu baada ya kifo chake kwa sababu hakukuwa na stakabadhi za kumtambua. Endapo angejulikana mapema, Walibora angehamishwa katika hospitali ya kibinafsi kwa sababu alikuwa na bima ya matibabu,” ripoti hiyo inaeleza.

Maseneta wanachama wa Kamati hiyo wanasema hata ingawa hospitali ya KNH haikuwa na lawama kwa kumtelekeza marehemu Prof Walibora, majeruhi wengi wa ajali za barabarani hufa katika hospitali hiyo ya rufaa kwa kukosa kuhudumiwa haraka.

Katika wasilisho lake mbele ya Kamati hiyo mnamo Aprili 15, 2020, Afisa Mkuu Mtendaji wa KNH Dkt Evans Kamuri alisema “Walibora aliletwa hospitalini mwendo wa saa tatu na nusu asubuhi (9.30am) mnamo Aprili 10, 2020, akipumua kwa ugumu”.

Wakati huo, Dkt Kamuri alisema, chumba cha kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali hiyo hakikuwa kimelemewa na idadi kubwa ya wagonjwa, ilivyodaiwa awali.

“Alipelekwa katika chumba B ambapo madaktari walijaribu kuokoa maisha yake kwa kumwongezea hewa ya oksijeni kwa kutumia mtambo maalum,” Dkt Kamuri akawaambia maseneta wakati huo.

Japo maseneta wametoa ripoti yao ya uchunguzi kuhusu kifo hicho cha Prof Walibora, polisi hawajatoa ripoti yao kuhusu kisa hicho kilichowaacha wengi na maswali chungu nzima.

Maelezo ya awali yalisema kuwa Prof Walibora aligongwa na gari alipokuwa akivuka barabara ya Landhies kwa mbio, akifukuzwa na wahuni Aprili 10, 2020 asubuhi.

Hata hivyo, haikujulikana ni shughuli zipi zilimpeleka katika maeneo ya kituo cha mabasi cha Machakos asubuhi ilhali alikuwa ameegesha gari lake katika barabara ya Kijabe, umbali wa kilomita mbili kutoka eneo la tukio.

Maafisa wa polisi hawajategua kitendawili kuhusu kifo cha Prof Walibora mwaka mmoja baadaye.

Marehemu ni mwandishi wa kazi nyingi za fasihi, maarufu miongoni mwazo ikiwa ni riwaya ya ‘Siku Njema’ iliyotahiniwa katika shule za upili kwa miaka mingi.

You can share this post!

Wadau waidhinisha mpango wa kupanua ushiriki wa UEFA kutoka...

Mshukiwa wa mauaji azuiliwa siku 14 Juja